2015-03-23 09:30:00

Ardhi ya Kanisa itumike kuzalisha chakula!


Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni limeamua kwamba, ardhi ya Kanisa ambayo haitumiki kwa sasa itolewe kwa wananchi ili waweze kuitumia kuzalisha mazao ya chakula kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo. Parokia mbali mbali nchini humo hazina budi kushiriki katika mchakato wa kupambana na baa la njaa Rwanda, kwani wakati wa njaa Kanisa linajikuta pia linawajibika kukabiliana na changamoto hii kama sehemu ya utume wake kwa Familia ya Mungu nchini Rwanda.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda linajiandaa pia kuadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini humo, maadhimisho yatakayofanyika tarehe 8 Septemba 2015. Kanisa pia linajiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 100 tangu Mapadre wa kwanza wazalendo walipopewa Daraja takatifu la Upadre. Hii itakuwa ni Jubilee ya Mapadre, itakayoadhimishwa tarehe 7 Oktoba 2017. Kanisa pia linaendelea kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa njia ya makongamano, tafakari na sala.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda, mwezi Mei litafanya mkutano kuhusu elimu, familia na amani. Jimbo Katoliki la Byumba, litakuwa ni mwenyeji wa Juma la Elimu Katoliki Kitaifa litakalofanyika tarehe 20 Juni 2015. Hii itakuwa ni fursa pia ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu wa Kanisa Anglikani nchini Rwanda kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene.

 

Maaskofu watapembua kwa kina na mapana dhamana ya familia katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani. Familia ya Mungu nchini Rwanda inaendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani. Askofu mkuu Luciano Russo anasema, watawa wana mchango mkubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.