2015-03-21 11:24:00

Wanawake wanahitaji: usawa, utu na haki msingi


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha usawa, utu na haki msingi za wanawake, ili kuwawezesha kutekeleza barabara dhamana na majukumu yao katika famia na jamii katika ujumla wake. Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa anachangia mada kuhusu kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mkutano wa Wanawake Kimataifa ulipofanyika mjini Bejing, China.

 

Utu na heshima ya mwanamke inapaswa kuzungumziwa kwa namna ya pekee katika mazingira ya maisha ya ndoa na familia na kwamba, wanawake wanayo dhamana kubwa ya kutunza na kuendeleza Injili ya Uhai, jambo ambalo linawawezesha kuishi katika utimilifu wao kama anavyobainisha Mtakatifu Yohane Paulo II.

 

Utu, heshima na upendo kwa wanawake ni mambo msingi yanayowawezesha wanawake kutekeleza dhamana yao kikamilifu, huku wakikamilishana na uwepo wa wanaume. Dhamana ya uzazi ni sehemu nyeti ya tasaufi ya maisha ya kiroho kwa mwanamke; hapa ni mahali ambapo anawajibika kuelimisha, kuonesha upendo wa dhati na kumfunda mtu kitamaduni. Kwa bahati mbaya, dhamana ya wanawake wengi katika jamii haiheshimiwi wala kuthaminiwa, kiasi cha kuwafanya wanawake kuishi njia panda kwa kuchagua jinsi ya kujikita katika maendeleo yao kama: wasomi na wafanyakazi; au kama wanawake na wazazi.

 

Askofu mkuu Bernadito Auza anakumbusha kwamba, mwanamke ana dhamana kubwa ya malezi na makuzi kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia; utume ambao wakati mwingine haupewi kipaumbele cha kwanza katika maisha ya wanawake wengi. Mwanamke na mwanaume wanakamilishana katika maisha na utume wao, kukataa uwepo wa tofauti hizi msingi ni kutaka kuichumia majanga Familia ya mwanadamu.

 

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kwa kuhakikisha kwamba, inalinda, inatunza na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Wanawake wafanyakazi walindwe na kupewa haki zao msingi. Kwa wale wanaotamani kupata watoto na kuwalea, wapewe nafasi hiyo, kwani ustawi na maendeleo ya binadamu unategemea kwa kiasi kikubwa sadaka na majitoleo ya wanawake ndani ya familia zao.

 

Askofu mkuu Bernadito Auza anasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na mila, desturi na tamaduni zilizopitwa na wakati kwa kuwabagua wanawake. Wanawake ni walimu wa kwanza wa imani, maadili na tunu msingi za maisha ya binadamu. Pale ambapo wazazi na walezi wanashindwa kutekeleza vyema dhamana yao katika malezi na makuzi ya watoto wao, hapo kuna ongezeko la uvunjifu wa sheria na mmong'onyoko wa kimaadili. 

 

Wanawake washirikishwe kikamilifu katika maisha ya jamii inayowazunguka, kwa kuwathamini na kuwajali kwani mchango wao katika ustawi na maendeleo ya mwanadamu hauna mbadala!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.