2015-03-21 15:34:00

Oyaaa! Tunataka kumwona Mnene!


Dili la Kumwona Kristo taaabu kweli kweli! Yoh. 12:20-33. Kituko kinachoelezwa katika Injili ya leo, kilitokea wakati wa Pasaka ya mwisho kabla ya ile aliyokufa Yesu. Wakati huo mji wa Yerusalemu ulikuwa na wakazi yapata arobaini elfu na wakati wa Pasaka idadi ya watu ilikuwa inaongezeka karibu mara tatu na hivi kufikia watu yapata laki moja na kidogo, kwa vile kipindi hicho walikuwa wanafika pia Wayunani au Wagiriki: “Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa wtu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu”.

 

Ukisikia jina hili Wayunani, kwa Myahudi ilimaanisha wageni, au watu wa kuja, yaani watu wasiokuwa Wayahudi. Kwetu wageni au wagiriki hao wanaitwa majina tofauti kadiri ya makabila. Wengine wanawaita wanyamahanga, au wagenzi, watu wa kuja. Waliweza kuitwa pia makafiri kwa sababu Wayunani hao hawakuwa wametahiriwa.

 

Wayunani hawa lakini walikuwa wanashabikia dini ya kiyahudi, na ikatokea kwamba baadhi ya Wayunani hao walitaka kumwona Yesu. “Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilea, wakamwomba wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwaona Yesu.” Suala la kushangaza ni kwamba, hawaendi wenyewe kumtafuta Yesu bali wanamwendea kwanza Filipo, ambaye naye anamtaarifu Andrea kisha pamoja wanaenda kwa Yesu. Filipo ni jina la asili ya Kiyunani (Kigiriki), kadhalika wafuasi hawa wote wawili walikuwa wanatoka Bethsaida kule Galilea mji uliokuwa mpakani mwa nchi ya Uyahudi na Ugiriki. Kwa vile mji wa Bethsaida ulikuwa kwenye mapito ya barabara kuu na ulikuwa mji wa biashara hivi kwa vyovyote ulikuwa mji uliochangamka sana na watu wake walikuwa wamefunguka macho.

 

Kwa hiyo Wayunani hao wakajisikia zaidi kumwendea Filipo kama mtoto wa nyumbani na kumwomba awafanyie "dili" la kumwona Yesu. Hapa neno hili “kuona” kwa kigiriki ni orao na maana yake ni “kuona kwa undani zaidi na kwa kina, yaani kuona kama ilivyokuwa kwa Zakeo aliyetaka kumwona Yesu, lilitumika pia neno hili "orao" siyo "blepo" lenye maana ya kuona kwa nje. Yaonekana Wagiriki hawa walikuwa na jambo moyoni na walitegemea kuwa Yesu peke yake ndiye angeweza kuwaondolea dukuduku lao ndiyo maana walitaka kumwona Yesu.

 

Ombi hili la Wagiriki yatakiwa liwe pia ombi letu. Tunaweza kuuona msalaba lakini hatupati ujumbe wowote ule, yaani hatuingii na kuona kwa undani orao. Kipindi cha Kwaresima ni mwafaka wa kuangalia kinaganaga ukweli wa Msalaba. Kuuona Msalaba na kuingia katika undani wake na kuuelewa Msalaba ni kiu gani.

 

Badala ya Filipo kwenda moja kwa moja kwa Yesu, naye anaenda kwanza kwa Andrea na wakiwa pamoja wanaenda kwa Yesu. Yawezekana mlolongo huo mrefu wa protokali ya kumwona Yesu na ya kumtambulisha yu nani kuwa ni dhamira kuu ya leo.

 

Yamaanisha kwamba kazi ya kutambulisha budi ifanyike na mtu anayefahamu kiundani na kinaganaga kile anachokitambulisha. Kwa hiyo mitume ndiyo wanaosadikiwa kuwa ndiyo waliomwelewa Yesu vya kutosha. Kwa vyovyote hilo linaeleweka kwani wao walishamwona na kumtambua Yesu kwa uhalisia wake, hivi sasa waliweza kumtambulisha kwa wengine. Fundisho ni hili kwamba hata sisi kama tumemwelewa Kristo kwa dhati tunaweza kumtambulisha kwa wengine, au tunaweza kumwelewesha Yesu kwa wengine endapo sisi wenyewe tunamwelewa kwa dhati.

 

Baada ya kumjulisha Yesu juu ya wayunani hao, sasa tungetegemea Yesu angeenda kuwaona Wayunani wale na kuwaamkia. Aidha mitume walimwuliza juu ya Wayunani, kumbe ukisoma kwa makini unaona kuwa jibu la Yesu ni nje kabisa ya swali na halifuati mantiki ya swali. Tungetegemea kwamba sasa Yesu anawaambia wafuasi wale, “Twendeni mkanioneshe ili niwaamkie na kuongea nao,” Kumbe yeye anaanza mara kuongea juu ya jambo jingine kabisa tena akiwaelekea mitume wale wawili na kuwajibu: “Umefika muda ambao mwana wa mtu atatukuzwa.” Hapa tunajifunza msamati mwingine muhimu “kutukuzwa” kwamba inabidi wamwone Mwana mtu aliyetukuzwa. Huyo ndiye mtu halisi aliyefaulu ndiyo maana sasa ametukuzwa.

 

Hapa tunapata ujumbe mkuu na muhimu sana, ni kwamba tukitaka kumwonesha Yesu, kwa wengine, yabidi kwanza kuuelewa ujumbe huu wa kumwona Kristo anayejionesha kwanza kwa  mitume. Wao ndiyo wanaotakiwa kumwona vizuri Yesu kabla ya kumwonesha kwa wengine. Kwamba Mwana wa mtu, aliyefaulu huyo ametukuzwa. Ni utukufu kwa vile amefikia kutoa kilele cha upendo wake wote.

 

Yesu anawaambia hawa mitume wawili, “umefika muda wangu.” Tunakumbushwa suala la muda au wakati katika arusi ya Kana Yesu alimwambia mama yake “Muda wangu haujafika.” Kadhalika pale wayahudi walipotaka kumshika lakini wanashindwa, Mwinjili anasema : “kwa vile haukuwa umetimia muda wake.” Kadhalika kabla ya kuoshwa miguu Mwinjili anasema: “Yesu akijua kwamba umewadia muda wa Pasaka.”

 

Katika Injili ya Yohana sura ya 17 “Padre umefika muda” yaani Pasaka yake, mateso huo ndiyo muda wa utukufu wake. Kwa hiyo kabla ya kumwonsha yesu kwa wengine yabidi kwanza wao mitume waone utukufu wa kweli wa yule anayetoa maisha. Usipoona hivyo huwezi kuona uhalisia wa Yesu Mwana wa Baba kwani utashindwa kumweleza jinsi alivyo. Kisha Yesu anaendelea bado kuwaeleza. “Chembe ya ngano isipoanguka katika archi inabaki kuwa peke yake, bali ikianguka hutoa mazao mengi.”

 

Kadhalaika akawaambia: “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele”. Sisi tunataka kutunza maisha haya ya kibaolojia, kumbe kinachofanyika ni kuitumia. Lakini kuchukia, yaani unapotoa yaonekana kama unachukia maisha kumbe ndiyo unayatunza. Mara nyingi watu wanaotoa maisha yao kwa ajili ya wengine wanakuja kusahaulika kabisa.

 

“Mtu akinitumikia, na anifuate, nami nilipo ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.” Kuwa mtumishi maana yake, ni kumpokea Yesu akiwa mtumishi. Jina hili mtumishi ni la kiheshima kabisa, mfano Musa anaitwa mtumishi wa Mungu, au Paul anaitwa kuwa mtumishi wa Kristu, au Maria ni mtumishi wa Bwana. Kwa sababu hawa ndiyo walioingia katika mipango ya upendo wa Mwana wake.

 

“Nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”  Yesu tutamkuta kwa mtu mwenye dhambi, kwa wagonjwa, kwa maskini. Kwa kila mtu mwenye shida, unashiriki kazi ya Yesu ya kutumikia ya kutoa maisha ya upendo kwa ajili yake huyo aliye pamoja na Kristu.  KristuYesu anaonesha historia yake yote katika mfano wa ngano mkate, ekaristi na divai kutoka zabibu. Yaani yabidi kujitoa kama hiyo punje ya ngano.

 

Hatima Yesu anasali: “Sasa roho yangu imefadhaika” Hata Yesu kama sisi, alikuwa woga wa kutoa maisha yake, mapema hivyo na kwa namna ile. Lakini hata hivyo alijitoa kwa ajili ya upendo. Ndipo sauti ikatoka mbinguni ikisema: “Nimelitukuza nami nitalitukuza tena.”

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.