2015-03-21 11:54:00

Mashirika ya Kimataifa yanapaswa kuzingatia sheria na kanuni


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaiomba Serikali ya Canada kuunda ofisi maalum itakayokuwa na dhamana ya kusikiliza kesi na malalamiko yanayotolewa na wananchi pamoja na makundi ya kutetea haki msingi za binadamu dhidi ya Makampuni ya Canada kimataifa, ili haki iweze kutendeka.

 

Kuna baadhi ya Makampuni ya Kimataifa kutoka Canada yanayoendelea kufanya hujuma za kiuchumi pamoja na kuvunja haki msingi za binadamu, lakini kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi katika nchi husika, makampuni haya hayafikishwei kwenye mkondo wa sheria, lakini wananchi wanaendelea kuhumia!

 

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM limemwandikia barua Askofu mkuu Paul-Andrè Durocher, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, ili kusaidia mchakato wa kuyafikisha mbele ya vyombo vya sheria kimataifa makampuni ya kimataifa kutoka Canada yanayokiuka sheria na haki msingi za binadamu wakati wanapotekeleza shughuli zao hasa kuhusiana na uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaendelea kuonesha mshikamano wake kwa Familia ya Mungu iliyoko katika Nchi za Amerika ya Kusini kutokana na madhara wanayokabiliana nayo kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta katika maeneo haya. Hivi karibuni, Maaskofu  wamesikilizwa na Tume ya Kimataifa ya Amerika ya Kusini, kuhusu haki msingi za binadamu, (CIDH).

 

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna makumpunu makubwa ya kimataifa yanayochimba madini na nishati mbali mbali Amerika ya Kusini, yenye usajili kutoka Canada; lakini kwa bahati mbaya, Mashirika haya yamekuwa ni chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, kiasi cha kusababisha madhara makubwa katika shughuli za uzalishaji na ukuaji wa uchumi katika maeneo haya. Faida kubwa inayopatikana kutokana na shughuli hizi za kiuchumi, haijaleta mafanikio makubwa kama inavyotarajiwa na watetezi wa haki msingi za binadamu.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakiri uwepo wa utata mkubwa kisheria huko Amerika ya Kusini kwa Makampuni yanayofanya shughuli zake huko, kumbe, kukiwepo na sheria makini katika nchi husika, Makampuni haya ya kimataifa yanaweza kuwajibishwa barabara. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kina kati ya wananchi na makampuni ya kimataifa pamoja na kufanya mageuzi makubwa katika mitazamo na vipaumbele vyao katika uzalishaji.

 

Maaskofu wanawachangamotisha wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi katika maeneo husika.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.