2015-03-21 12:28:00

Haki haiwezi kupatikana kwa njia ya adhabu ya kifo


Maisha ya binadamu ni matakatifu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, hakuna haki inayoweza kupatikana kwa njia ya mauaji na kwamba, adhabu ya kifo imepitwa na wakati haistahili kuendelea kuwepo. Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na  ujumbe wa Tume ya Kimataifa dhidi ya adhabu ya kifo, ilipomtembelea mjini Vatican, Ijumaa tarehe 20 Machi 2015.

 

Adhabu ya kifo ni ukatili usiokuwa na kifani na kwamba, kuna adhabu mbadala zinaweza kutumika ili kulinda, kutetea na kuheshimu zawadi ya uhai na kwamba, mauaji ya mkosaji hayawezi kusaidia kuimarisha haki kwani haki inapatikana pale mkosaji anapotambua kosa na kupata nafasi ya kutubu na kubadilika ili aweze kuwa mtu mwema zaidi.

 

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa itafuta adhabu ya kifo kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kielelezo cha upendo mkamilifu wa Mungu kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu hafurahii kifo cha mkosaji, bali apate nafasi ya kutubu na kuongoka, hata kwa mkosaji bado hadhi yake kama binadamu iko pale pale.

 

Adhabu ya kifo ni kwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu; adhabu ya kifo inakinzana na huruma ya Mungu kwa binadamu; wakati wa kusubiri utekelezaji na wakati wa utekelezaji wa adhabu yenyewe. Hukumu ya adhabu ya kifo ni mchakato unaochukua muda mrefu zaidi hadi kufikia utekelezaji wake, jambo ambalo linasababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa mkosaji.

 

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, mara nyingi adhabu ya kifo inatolewa na Serikali zinazowaongoza watu wake kwa mabavu kama njia ya kuwanyamazisha; ni adhabu ambayo inatumiwa na watu wenye misimamo mikali ya kiimani na kijamii, mara nyingi kwa ajili ya mafao yao binafsi, kama hali inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kuzalisha makundi makubwa ya Wafia dini. Haki kamwe haiwezi kupatikana kwa njia ya mauaji ya binadamu.

 

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutafuta adhabu mbadala kwa watu wanaopatikana na makosa ambayo adhabu yake ni hukumu ya kifo; ili hata watu hawa waweze kuonja tena katika maisha yao, huruma na upendo wa Mungu; uhuru na matumaini mapya.

 

Hii ni changamoto kwa Serikali mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, zinafanya maboresho makubwa katika mfumo wa magereza yake kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.