2015-03-21 11:44:00

Changamoto za COMESE Barani Ulaya


Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Jumuiya ya Ulaya, COMECE, imehitimisha mkutano wake hivi karibuni, uliojadili pamoja na mambo mengine fursa za ajira, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kanuni maadili. COMECE inatarajiwa kufanya mkutano wake wa mwaka kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 29 Oktoba 2015 huko Paris, Ufaransa. Wajumbe wa mkutano wamemchagua tena Kardinali Reinhard Marx kuongoza Tume hii kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

Tume ya COMECE inafuatilia kwa umakini mkubwa mazungumzo juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linapenda kuchangia mawazo yake katika maadhimisho ya mkutano wa kimataifa utakaojadili athari za mabadiliko ya tabianchi (Co21) Desemba, 2015 huko Paris, Ufaransa.

Tume hii inaendelea kushirikiana kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani ili kuhusiana na uchumi na biashara; uwekezaji, mafao ya wengi, fursa za ajira pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Majadiliano kati ya pande hizi mbili yataendelea kujadiliwa katika kipindi cha miaka mitatu na hatimaye kuonesha msimamo na mchango wao kwa Jumuiya ya Kimataifa. Maaskofu wanaendelea kukazia pia ushirikishwaji wa Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya ushirikiano wa kidugu na umoja.

Maaskofu wa COMECE wanasikitishwa sana kutokana na ongezeko la vitendo vya kigaidi, ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana pamoja na ongezeko kubwa la wahamiaji; mambo yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kumong'onyoka kwa maadili na utu wema; athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na majanga asilia. Kuna idadi kubwa ya wakristo wanaoendelea kuteswa na kunyanyaswa huko Mashariki ya kati. Hapa Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na haki msingi ya uhuru wa kidini.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.