2015-03-21 12:17:00

Askofu ni kiongozi wa wote!


Askofu katika maisha na utume wake anapaswa kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu ambao amekabidhiwa na Mama Kanisa, ili kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ajitahidi kuhakikisha kwamba, anawavuta watu kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Yesu Kristo kwa njia ya ushuhuda makini, wenye mvuto na mashiko.

 

Huu ni wosia uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 19 Machi 2015, alipokuwa anamweka wakfu Askofu mkuu Joel Mercier, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa viongozi wa Kanisa kutoka ndani na nje ya Vatican pamoja na Familia ya Mungu katika ujumla wake. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la "San Luigi dei Francesi" lililoko Jimbo kuu la Roma.

 

Kardinali Parolin amemtaka Askofu mkuu mpya kuhakikisha kwamba, katika maisha na utume wake, anaongozwa na Mwenyezi Mungu, daima ajitahidi kuwa mnyenyekevu na mwajibikaji kwa karama mbali mbali ambazo amekirimiwa na Roho Mtakatifu. Akumbuke kwamba, kwa sasa ni chombo cha kazi ya Roho Mtakatifu na chemchemi ya maji safi yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

 

Uaskofu ni dhamana inayojikita katika huduma kwa Familia ya Mungu na wala si kielelezo cha madaraka, ufanisi katika maisha ya Kikasisi wala utukufu wa mtu binafsi. Askofu anawajibika kujenga na kuimarisha mahusiano yake na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na urika wa Maaskofu wenzake. Askofu ajitahidi kuonesha moyo wa huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo.

 

Kardinali Pietro Parolin, amempongeza Askofu mkuu Joel Mercier kwa huduma makini ambazo ameendelea kuzitoa kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu, kiasi hata cha kuweza kujimwilisha katika historia, jiografia na tamaduni za watu mbali mbali. Sasa amepewa dhamana ya kujenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo, kwa njia ya mahubiri yanayojikita katika ushuhuda wa maisha; kuwatakatifuza Watu wa Mungu na kuwaongoza kwa kumuiga Yesu Kristo mchungaji mwema.

 

Kama Askofu ajitahidi kuwatafuta Kondoo waliopotea, kwa kuwapenda, kuwajali na kujisadaka maisha yake kwa ajili yao. Askofu awe ni mtu wa sala kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.