2015-03-20 09:59:00

Uhuru wa kidini una maana pana zaidi!


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu uhuru wa kidini, "Dignitatis Humanae", linalojadili kuhusu haki ya mtu binafsi na ya jumuiya ya kuwa na uhuru wa kijamii na kiserikali katika masuala ya dini.

 

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican wanabainisha wazi kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubaliwa kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni utu na hadhi ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, uhuru wa kuabudu ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu.

 

Askofu mkuu Charles Chaput, wa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, hivi karibuni wakati akichangia mada kwenye semina kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Tamko la Uhuru wa Kidini anabainisha kwamba, nchini Marekani kuna shinikizo kutoka katika makundi ya kijamii yanayoitaka Serikali kuachana na Mapokeo ya uhuru wa kidini.

 

Lakini, ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini una maana kubwa zaidi kwani ni fursa kwa waamini wa dini mbali mbali kusali, kufundisha na kushuhudia imani yao katika maisha ya hadhara na binafsi. Uhuru wa kidini unamaanisha wazazi na walezi kuwa na haki ya kuwalinda na kuwasimamia watoto wao dhidi ya elimu inayoweza kuathiri malezi na makuzi yao pamoja na kutoa nafasi kwa dini mbali mbali kushiriki kikamilifu katika kuwafunda watu kanuni maadili na utu wema sanjari na kuendelea kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji zinazofanywa na dini mbali mbali. Mababa wa Mtaguso walitaka yote haya yatekelezwe kikamilifu pasi na kuingiliwa na Serikali.

 

Askofu mkuu Chaput anabainisha kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanaomchango mkubwa katika ujenzi na ustawi wa nchi yao na kwa namna ya pekee, wananchi wengi wa Marekani wana imani kwa Mwenyezi Mungu na wengi wao wanajipambua kuwa ni Wakristo. Lakini mambo yanaendelea kubadilika kwa kasi ya ajabu, vijana hawapendi tena mambo ya kidini na wala hawaelewi kwa undani zaidi maana ya uhuru wa kidini katika maisha na tamaduni za watu.

 

Askofu mkuu Chaput anakumbusha kwamba, wanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini mwanadamu amekuwa ndiye mvunjaji mkubwa wa uhuru wa kidini kwa kutozingatia dhamiri nyofu; kwa kukumbatia utamaduni wa kifo au kwa ufundishaji wa ngono shuleni! Mambo ya kusikitisha sana. Watu wanataka kufuta tofauti za kijinsia kwa kudhani kwamba, hii ni haki yao msingi. Mwanadamu anapaswa kutambua kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

 

Askofu mkuu Chaput anashutumu tabia ya kulazimisha watu kujiunga na dini fulani kwa kitisho cha mtutu wa bunduki au jambia na kusahau kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inapaswa kupokelewa kwa unyenyekevu na ukweli. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani yao katika matendo vinginevyo, inakuwa vigumu sana kwa Katiba ya nchi kuwalinda na kuwatetea wananchi wake. Wananchi watambue maana ya uhuru wa kidini na kuendelea kuukumbatia kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.