2015-03-20 15:18:00

Kardinali O'Brien wa Scotland avuliwa madaraka


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kuvuliwa dhamana na madaraka ya Ukardinali yaliyowasilishwa kwake na Kardinali Keith Michael Patrick O'Brien, Askofu mkuu mstaafu wa Saint Andrews na Edinburg, Scoltland, mintarafu sheria za Kanisa Namba 349, 353 na 356.

 

Kwa uamuzi huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Familia ya Mungu nchini Scotland na anapenda kuwatia moyo waendeleze mchakato wa upyaisho wa maisha na upatanisho wa kweli.

 

Itakumbukwa kwamba, Kardinali O'Brien baada ya kufanya majadiliano ya kina na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwezi Mei 2013, alimpatia nafasi ya kutubu, kufunga, kusali na kutafakari kuhusu maisha na utume wake kama Kasisi wa Kanisa na baadaye kukiri mwenyewe udhaifu wake wa kibinadamu dhidi ya maisha na utume wake kwanza kabisa kama Padre, Askofu na Kardinali.

 

Kutokana na mwelekeo huu, Kardinali O'Brien wakati huo, aliomba radhi kwa Familia ya Mungu na Kanisa kwa ujumla nchini Scotland. Tangu wakati huu ameamua kujichimbia katika maisha binafsi na kamwe hataweza kushiriki tena shughuli za hadhara. Itakumbukwa kwamba, Kardinali O'Brien hakushiriki kwenye mkutano wa Makardinali kwa ajili ya kumchagua Papa Francisko.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.