2015-03-20 09:05:00

Jiandaeni vyema kuadhimisha Fumbo la Pasaka


Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe,  (CECCI) katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2015 linawataka waamini kuwa na busara, kupima na kutenda kila jambo kwa ujasiri, weledi, toba na wongofu wa ndani. Waamini wahakikishe kwamba, wanajiandaa vyema kuadhimisha Fumbo la Pasaka, huku wakiwa wamejitakasa kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kukumbatia neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.

 

Maaskofu wanawataka waamini kujenga moyo wa amani na utulivu wa ndani kwa kuepukana na vishawishi mbali mbali vinavyoweza kuwapotosha na kuwaweka mbali na kweli za Kiinjili. Waamini waonesha ukomavu katika maamuzi yao bila kuyumbishwa na kelele za mitaani. Wasikilize kwa makini kila ambacho Mama Kanisa anafundisha, kwani Yeye ni Mama na Mwalimu anayodhamana ya kuwaonesha waamini njia nyofu inayokumbatia kweli za kiimani, maadili na utu wema. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni mtetezi mkuu wa utu na heshima ya binadamu; mazingira; mafao, mafao ya wengi, maendeleo na ustawi wa jamii.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, linapenda kuwaalika waamini kuwa makini na Ibada potofu kwa Bikira Maria; Ibada ambazo zinalenga kuwajengea waamini hofu kwa kutumia mitandao ya kijamii. Waamini wajitahidi kufahamu kweli za Kiinjili, maadili na utu wema; wawe mashuhuda kweli wa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo.

 

Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, wanaialika Familia ya Mungu nchini humo, katika kipindi hiki cha Kwaresima: kutafakari Neno la Mungu, kusali, kufunga na kutoa sadaka kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Familia ya Mungu itambue kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kila mtu aokoke na kuingia katika Ufalme wa mbinguni, wala hafurahii kifo cha mwenye dhambi, bali atumie muda wake kwa kutubu na kumwongokea Mungu.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, linaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali bila kuchoka kwa ajili ya kuombea haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Maaskofu wanahitimisha ujumbe wao wa Kwaresima kwa kumwomba Bikira Maria, Malkia wa amani na msimamizi wa Nchi ya Pwani ya Pembe, ili kwamba, kwa njia ya maombezi yake, asaidie kuimarisha nguvu ya waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.