2015-03-20 08:52:00

Chagueni viongozi wakweli, waaminifu na wachamungu


Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawajibika katika utekelezaji wa dhamana yao ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba 2015.

 

Familia ya Mungu nchini Argentina ihakikishe kwamba: haki, amani na utulivu vinatawala, ili wananchi waweze kutekeleza haki yao kikatiba bila ya vitisho wala vurugu. Ikumbukwe kwamba, uchaguzi mkuu ni utekelezaji wa demokrasia inayowapatia wananchi uhuru wa kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi yao kwa kuwajibika kikamilifu wakati wa kupiga kura.

 

Maaskofu Katoliki Argentina wanaitaka Familia ya Mungu nchini humo kujikita katika misingi ya kuheshimiana, ili kukoleza majadiliano yanayojengeka katika ukweli na uwazi ili kutafuta mafao ya wengi ili hatimaye, kufikia malengo yanayokusudiwa. Jamii inahitaji viongozi watakaosaidia mchakato wa kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu kwa kuongeza fursa za ajira; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki zake msingi pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini.

 

Viongozi watakaochaguliwa wawe ni watu wanaojipambanua kwa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti inapomfika. Wasiwachague viongozi wanaokumbatia utamaduni wa kifo, watawaletea majanga katika maisha kwa siku za usoni. Wananchi wawachague viongozi wenye usongo wa maendeleo katika sekta ya elimu na maboresho katika masuala ya uchumi, kwa kuongeza bidii katika ukuaji wa sekta ya uchumi pamoja na kupunguza mfumko wa bei ya bidhaa na huduma inayotolewa nchini Argentina.

 

Ili kweli malengo haya yaweze kufikiwa, kuna haja ya kuwa na viongozi wachamungu, wakweli na waadilifu; watu makini katika maisha na kauli zao; watu ambao si wabinafsi, wala rushwa wala mafisadi. Watu kama hawa hawana nafasi ya kupewa dhamana ya kuongoza nchi.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema na uzalendo kwa nchi yao kuwapima na hatimaye, kuchagua watu makini si kutokana na umaarufu wa Chama, mahali au dini ya mtu; wawe ni viongozi wanaowajibika na wenye historia nzuri katika maisha; waaminifu na wakweli; watu wenye uchungu wa maendeleo kwa watu wao. Viongozi hawa ndio watakaosaidia kumwilisha haki, amani, ukweli na uhuru, mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya nchi.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema na uzalendo kwa nchi yao, kuchagua viongozi wenye utamaduni wa kujadiliana; watu wanaoweza kusikiliza na kusikilizwa; ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano na uwajibikaji nchini Argentina.

 

Viongozi watakaochaguliwa, wasaidie mchakato wa kujenga ukweli, haki, uhuru, mshikamano na upatanisho, ili kweli taifa liweze kuimarisha umoja na mfungamano wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linahitimisha ujumbe wake kwa Familia ya Mungu nchini humo kwa kuitaka kusimamia ukweli, haki na amani.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.