2015-03-19 12:17:00

Mfuko wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani amewaandikia barua wanadiplomasia na wadau mbali mbali ili kuunga mkono juhudi za Vatican katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi, kwa kuwasaidia waathirika kwa hali na mali kwa kutambua kwamba, kwa sasa kuna umati mkubwa wa watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi.

 

Vatican tayari imekwishachangia kiasi cha Euro laki tano na wafadhili mbali mbali wanaendelea kuchangia katika mfuko huu maalum, lengo ni kuwa na kiasi cha Euro millioni tatu zitakazosaidia katika mapambano ya ugonjwa wa Ebola ambao umesababisha majanga makubwa kwa wananchi wa Afrika Magharibi. Lengo ni kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati na waathirika wa ugonjwa wa Ebola kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muda wa kuonesha imani tendaji kwani maneno matupu yamepitwa na wakati.

 

Baraza la Kipapa la haki na amani linataka kushikamana na Familia ya Mungu Afrika Magharibi ili kusaidia kupambana kikamilifu na athari za ugonjwa wa Ebola. Fedha zinazochangwa kwa wakati huu, zinapania kuboresha miundo mbinu ya hospitali ili kuwahudumia vyema zaidi wagonjwa wa Ebola. Pili ni kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kuwapatia elimu na huduma msingi kama chachu ya matumaini kwa siku za usoni.

 

Kardinali Peter Turkson anasema kwamba, lengo la tatu la Mfuko wa Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola ni kusaidia mchakato wa majiundo kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ili kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ebola kwa kukazia usafi wa mazingira na maisha ya watu. Nne, mfuko huu utawasaidia Wakleri kutekeleza vyema mikakati na sera za kichungaji kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola.

 

Mfuko huu unaendelea kuchangiwa na Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa na kitaifa. Mabaraza ya Maaskofu mahalia yameonesha pia nia ya kuchangia mfuko huu kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola, Afrika Magharibi.

 

Kardinali Peter Turkson anaishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, Afrika Magharibi. Mfuko wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola unasimamiwa na wajumbe watano ambao wako chini ya Kardinali Peter Turkson. Kwa Mashirika ya Kitawa pamoja na watu binafsi wanaweza kufanya hivyo hadi mwishoni mwa mwezi Aprili, ili mikakati iliyopangwa ianze kufanyiwa utekelezaji wa dhati bila kuchelewa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.