2015-03-19 15:24:00

Endeleeni kupandikiza mbegu ya majadiliano ya kidini!


Ni Jambo la kusikitisha sana kuona kwamba, dini inatumika kwa ajili ya kuhalalisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na kwamba, ni jambo lisilokubalika kimaadili watu kutengwa kutokana na: dini, imani au makabila yao; haya ni mambo ambayo yanasababisha chuki, kinzani na misigano mikali ya kijamii. Hii ni changamoto kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuendelea kushikamana kwa dhati ili kuhakikisha kwamba, inaendelea kupandikiza mbegu ya majadiliano ya kidini, hata kama itachukua muda mrefu kutoa matunda yanayokusudiwa na wengi.

 

Haya yamesemwa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, Jumatatu tarehe 16 Machi 2015 wakati alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kichungaji nchini Pwani ya Pembe, iliyomwezesha kukutana na kuzungumza na Familia ya Mungu nchini humo wakati huu, inapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha miaka 110 tangu Ukristo ulipoingia nchini Pwani ya Pembe.

 

Wakristo na Waislam hawana budi kuendeleza majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi; haki na amani; majadiliano yanayojikita katika maisha ya waamini na tasaufi yao; kwa kutoa nafasi kila upande kushuhudia imani yake na kukazia mambo yanayowaunganisha zaidi kuliko kuendeleza malumbano na misigano isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi watu. Vijana wafundwe kutambua kwamba, hata katika dini na jamii ya wengine kuna mambo mema na matakatifu yanayopaswa kuheshimiwa na kudumishwa.

 

Moyo wa mwanadamu unafumbata siri kubwa ya vita na kinzani, lakini pia ni chemchemi ya haki, amani na upendo. Familia ya Mungu Barani Afrika haina haja ya kukata tamaa kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika majadiliano ya kidini, bali waendelee kuwa na imani na kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwakwamua kutoka katika woga usiokuwa na msingi, ili wote kwa pamoja waweze kuonja furaha, amani na utulivu, kwa kuheshimiana hata katika tofauti, ili kujenga na kudumisha umoja na maridhiano ya kweli.

 

Kardinali Tauran anawataka Wakristo Barani Afrika kuendelea kuimarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pasi na woga, kwa kujenga umoja na mshikamano; kwa kuendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni. Ukristo ni dini ambayo inajikita katika maisha ya watu wanaotaka kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka anawakirimia waja wake mwelekeo mpya wa maisha.

 

Kardinali Tauran na ujumbe wake, wamepata pia fursa ya kukutana na Rais Alassane Outtara. Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini amekumbusha kwamba, Kanisa katika maisha na utume wake, linapenda kuheshimu waamini wa dini zote. Huu ni mwaliko pia kwa waamini wa dini nyingine kujifunza kusaidia kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, zitakazowawezesha waamini kufanya mageuzi ya ndani katika maisha yao.

 

Haya yanawezekana pale ambapo kuna uhuru wa kidini unaojikita katika ukweli na uwazi na kwamba, kila dini inapaswa kusaidia kuimarisha umoja, udugu na mshikamano wa upendo badala ya kuwa ni kichocheo cha vita, chuki na vurugu kati ya jamii. Waamini wa dini mbali mbali wanachangamotishwa kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya amani duniani.

 

Tofauti zao msingi ni utajiri mkubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya mwanadamu. Kuna haja ya kuvuka mipaka ya maridhiano na kuanza kukazia zaidi: heshima, upendo na amani.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.