2015-03-19 15:49:00

Boko Haram chanzo cha majanga ya kudumu Nigeria


Viongozi wa kidini nchini Nigeria wanabainisha kwamba, haitakuwa rahisi sana kwa wananchi wengi wa Nigeria kusahau kwa haraka: adha, madhara na athari zilizosababishwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram, hasa Kaskazini mwa Nigeria. Kumbe, kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, licha ya kudhibiti vitendo vya kigaidi vya Boko Haram, lakini nchi pia inapaswa kuanza mchakato wa uponyaji na upatanisho wa kitaifa ili kuwajengea tena wananchi wa Nigeria amani na maridhiano; tayari kuanza kufungua ukurasa mpya wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa kitaifa.

 

Haya ni kati ya mambo yaliyobainishwa wakati wa kongamano la majadiliano ya kidini lililokuwa limeandaliwa huko Afrika Magharibi, ili kuangalia kwa kina na mapana athari na changamoto za misimamo mikali ya kidini na kiimani miongoni mwa jamii ya watu. Kongamano hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kidini kutoka Nigeria.

 

Viongozi wamelaani mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram nchini Nigeria, lakini yakiwa na malengo mapana zaidi kimataifa. Kuibuka kwa Boko Haram ni matokeo ya: Udini na misimamo mikali ya kidini; rushwa na ufisadi; utawala mbaya na wahusika kutofikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa wakati muafaka hasa miongoni mwa wasomi wengi wa Nigeria.

 

Hata kama Boko Haram itadhibitiwa kikamilifu madhara yake ni makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Nigeria. Wamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; wamejenga hofu na utengano miongoni mwa wananchi wa Nigeria. Waswahili husema, usipoziba ufa utajenga nyumba!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.