2015-03-17 12:23:00

Shikamaneni kupinga itikadi kali za kiimani Barani Afrika


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Yamoussoukro, Pwani ya Pembe, Jumatatu tarehe 16 Machi 2015, ameiambia Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe kwamba, Kanisa linawaheshimu waamini wa dini mbali mbali kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanazo haki zao msingi na kwamba, kile wanachokiamini ni chema na kitakatifu.

 

Akiwa nchini humo, Kardinali ameshuhudia mwenyewe tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii zinavyodumishwa na waamini wa dini mbali mbali, katika misingi ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Kwa njia ya wazee, vijana wanarithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho zinazojikita katika imani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia, ambaye ni mwema na mwenye haki, changamoto kwa waamini kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

 

Kardinali Tauran anasema, historia ya wananchi wa Pwani ya Pembe inaonesha kwamba, kumekuwepo na misigano mikubwa ya kiimani katika nchi hii, changamoto kwa waamini wote ni kujitahidi kuwa kweli ni vyombo vya upatanisho, haki na amani; kwa kushirikiana na kushikamana ili kung'oa kabisa ubaguzi, chuki, utengano na misimamo mikali ya kidini inayopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mikakati hii inaweza kufanikiwa kwa njia ya elimu makini, kwa kupokea na kukubali tofauti zilizopo kuwa ni sehemu ya utajiri wa Familia ya Mungu; ili kujenga urafiki na udugu kwa ajili ya mafao ya wengi.

 

Kardinali Tauran, Jumapili tarehe 15 Machi 2015 ameadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 110 tangu Ukristo ulipoingia kwa mara ya kwanza nchini Pwani ya Pembe, kwa njia ya Mlango wa Korhogo, Parokia iliyoko Kaskazini mwa nchi. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza Wamissionari, Makatekista na Wasaidizi wao waliowezesha mchakato wa Uinjilishaji kupenyeza katika maisha na vipaumbele vya watu, leo hii Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 110 ya Uinjilishaji.

 

Kwa namna ya pekee, Kanisa linawakumbuka Watumishi wa Mungu: Louis Houandete na mke wake Valeria Amah. Huu ni mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini humo kuendelea kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo pamoja na kujikita katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, kama ilivyofanya mihimili ya Uinjilishaji, miaka mia moja iliyopita. Waamini wanaalikwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambuana kama ndugu na wala si maadui; ya kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti mbali mbali zinazoweza kujitokeza, daima wafanye yote kwa mwanga wa Injili.

 

Waamini watambue na kukiri mapungufu yao ya kibinadamu, tayari kukimbilia upendo, huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kujenga na kudumisha: imani, matumaini na mapendo. Waamini watambue kwamba, hata wale ambao hawamwamini Mungu, lakini Mungu ana imani nao. Bado kuna idadi kubwa ya Wakristo anasema Kardinali Tauran wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa linashuhudia umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.