2015-03-17 14:24:00

Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutangaza rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Huruma ya Mungu, Siku iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Maadhimisho rasmi tafunguliwa tarehe 8 Desemba 2015 na kufungwa rasmi tarehe 20 Novemba 2016, Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Dunia. Hiki ni kipindi cha maadhimisho ya Jubilee ya huruma ya Mungu.

 

Wakati huo huo, Shiriko la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kuanzia tarehe 29 Julai 2015 hadi tarehe 29 Julai 2016 linaadhimisha Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika. Tamko hili limetolewa na Kamati kuu ya SECAM katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni mjini Windhoek, Namibia. Kanisa Barani Afrika halina budi kutaja dhambi na mapungufu yake kwa majina bila kuogopa, ili kuliwezesha Kanisa kuanza mchakato wa upatanisho wa kweli Barani Afrika.

 

Itakumbukwa kwamba, hii ni changamoto ambayo ilitolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, Dhamana ya Afrika, Africae Munus kwa kuwajali watu, jambo ambalo linahitaji wongofu wa kweli, yaani "metanoia". Huu ni mwaliko wa kuuishi ukweli wa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho, kwa kujenga ari na moyo wa umoja na upatanisho kati ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

 

Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na utamadunisho wa Injili na Uinjilishaji wa utamaduni sanjari na kuzingatia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Kristo kwa ajili ya Kanisa lake. Hapa waamini wanajichotea utajiri wa Neno la Mungu na chakula cha njiani, tayari kumshuhudia Kristo aliye chemchemi ya neema na upatanisho kati ya Mungu na binadamu na kati ya mwanadamu na jirani yake. Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu sanjari na Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, iwe ni chemchemi ya neema na baraka kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.