2015-03-17 12:05:00

Kwaresima ni kipindi cha mshikamano wa upendo na udugu


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoendelea kuteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia. Maaskofu wanasema, Wakristo huko Mashariki ya Kati wanateseka sana, kiasi hata cha kukata tamaa ya maisha.

 

Kipindi cha Kwaresima, ile ni fursa ya kuwakumbuka, kuwaombea na kuwasaidia kwa hali na mali Wakristo huko Mashariki ya Kati kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo, udugu na mshikamano. Watambue kwamba, hata katika mahangaiko na mateso yao ya ndani kuwa ndugu zao katika Kristo wanaoendelea kuwaenzi. Hii ni changamoto ambayo inatolewa na Askofu mkuu Joseph Edwars Kurtz kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

 

Kwaresima ni kipindi cha: Sala, toba na wongofu wa ndani; ni muda muafaka wa kutafakari kwa kina Neno la Mungu pamoja na kujikita katika Sakramenti za Kanisa zinazomwezesha mwamini kupta rehema na neema katika hija ya maisha yake ya kiroho; changamoto ya kumwilisha imani katika matendo ya huruma. Kwaresima iwe ni fursa kwa waamini kuungana na watu wanaoteseka na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, majanga asilia pamoja na kinzani za kidini na kijamii, ili waendelee kuwa na matumaini kwamba, iko siku wataweza kuona mwanga wa haki na amani ukiwashukia na kuwaangazia ili waweze kupata furaha ya kweli.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaungana kwa dhati kabisa na Baba Mtakatifu kulaani nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Wanaiomba Serikali ya Marekani kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu mintarafu sheria za kimataifa, utu na heshima ya binadamu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahii ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.