Baba Mtakatifu Francisko, katika kipindi hiki cha Kwaresima, amewaandikia barua ndugu zake Maaskofu Katoliki wa Nigeria, ambamo ameomba pia wafikishe salaam zake kwa Jumuiya za Kikristo walizopewa dhamana katika huduma za kichungaji, akionesha mshikamano na mawazo yake kwa hali ngumu na changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa.
Katika barua hiyo, Papa amesema, “wakati huu tunapotembea kuelekea ufufuko wa Yesu Kristo tukiwa tumeungana pamoja na Kanisa zima, ninapenda kutoa saalam zangu za dhati , kwenu nyote Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa Nigeria na pia naomba mzifikishe kwa jamii Kikristo mliyokabidhiwa katika huduma ya kichungaji. Aidha ninapenda kushirikishana nanyi, baadhi ya mawazo yangu kuhusu hali halisi za sasa za maisha katika nchi yenu”.
Barua ya Papa, imeendelea kuitaja nchi ya Nigeria, taifa kubwa kuliko yote Barani Afrika, yenye kuwa na raia zaidi ya milioni 160, yenye kujulikana kama kinara si Barani Afrika tu lakini duniani kote.
Papa ametaja kwa jinsi taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni limeweza kushuhudia ukuaji wa haraka wa uchumi na pia kwa mara nyingine kujiwasilisha katika jukwaa la kimataifa kama soko la kuvutia, kutokana na uwepo wa rasilimali, na kwa uwezo wake wa kibiashara. Na pia kwa jinsi linavyojitambulisha lenyewe kuwa mtendaji mkuu katika utatuzi wa migogoro ya kisiasa Barani Afrika.
Lakini wakati huohuo, taifa lao linakabiliwa na matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na aina mpya ya vurugu za kuvuka mipaka na misimamo mkali inayoendeshwa kwa misingi ya kikabila, kijamii na kidini, ambamo kwayo Wanigeria wengi wameuawa, kujeruhiwa na kuwa vilema; kutekwa na kupokonywa kila kitu si mali tu lakini hata na wapendwa wao, nchi yao, maisha yao, utu wao na haki zao. Watu wengi hawawezi kurudi makwao. Wote sawia: Wakristo na Waislamu, wanayapita mateso haya makubwa kama matokeo ya wachache wanaodai kuwa watu wa dini zaidi, ambao hulitumia jina la dini vibaya kwa kutengeneza itikadi zao za kidini kwa maslahi yao kupitia dhuluma na vifo.
Katika hali hizo, Papa anapenda kuwahakikishia kwamba yu karibu na Maaskofu na wale wote wanaoishi mateso na unyanyasaji huo. Na kwamba kila siku anawakumbuka katika sala zake nakwa mara nyingie anapenda kuwatia shime na faraja kwa maneno ya kufariji ya Yesu Kristo, yanayopaswa kusikika daima ndani ya moyo wa kila mmoja: "Nawaachieni amani, amani yangu nawapa" (Yoh 14:27).
Amani, Papa ameendelea kusema, si tu kutokuwa na vita au kama matokeo ya kukosekana kwa maelewano katika baadhi ya vipengere vya kisiasa, au ukosefu wa ubabe wa kupindukia. Lakini Amani, ni kwa ajili yetu, ni zawadi inayotoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, Mfalme wa amani, anayewafanya wawili kuwa sawa na mtu mmoja( Efe. 2:14). Na ni tu wale wenye kupokea amani ya Kristo ndani ya mioyo yao na kuihifadhi, kama mwanga wa kuwaongoza katika njia ya maisha wanaweza kuwa wajenzi wa amani (Rej. Mt 5,9.).
Wakati huo huo, amani ni utendaji wa kila siku, wa kijasiri na halisi ya kukuza maridhiano na ushirikiano katika uzoefu wa maisha, kupanua ujenzi wa madaraja ya majadiliano, huduma kwa wanaoishi mazingira magumu na wanyonge zaidi waliotengwa. Kwa neno moja, amani ni ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana.
Katika Barua hii, Papa pia anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Maaskofu, kwa sababu katikati ya majaribu mengi na mateso, Kanisa nchini Nigeria, limeendelea kuhudumia kwa ukarimu, huruma na msamaha. Na hivyo, amewakumbuka Mapadre, watawa na makatekista ambao licha ya kuhatarisha maisha yao, hawatelekezi kundi lao, bali wanaendelea kubaki imara katika utumishi wao, huku wakihubiri na kuendelea kuwa waamini kwa Injili ya Kristo.
Kwao wote, Papa ametoa shukrani zake za dhati na kuonyesha mshikamano wake, na kuwataka wasichoke kutenda mema. Kwa ajili yao alitolea shukurani ka Bwana pia kwa watu wengi toka pande mbalimbali za kijamii, kiutamaduni na kidini ambao kwa mapenzi yao na maamuzi yao thabiti, wamesimama imara kupinga kila aina ya ghasia na fujo, na kwa wale wote wenye kupendelea neema ya usalama na utulivu kwa ajili ya wote.
Watu hao wanakuwa ni mfano mzuri unaotutia nguvu mpya ya kusonga mbele katika kushuhudia manufaa ya amani kama Papa Mstaafu Benedikto wa XVI, alivyokumbusha mwishoni mwa Sinodi kwa ajili ya Afrika, Ni nguvu ya Roho Mtakatifu ambayo hubadilisha mioyo ya waathirika na watesaji wao na hivyo kuweza kurejesha udugu" Dhamana ya Afrika, (Africae Munus, 20) .
Kwa maono haya Papa Francisko amewahimiza ndugu zake Maaskofu wa Nigeria, kudumu katika uvumilivu na bila kukata tamaa, bali kusonga mbele pamoja katika njia ya amani (Rej Lk 1:79.) na katika kuwaongoza waathirika, kuwasaidia maskini na kuelimisha vijana ili wote waweze kuwa ni vyombo vya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.
Mwishoni, Papa Francisko kupitia barua hii amewapatia baraka zake za Kitume, akiwataka pia wazifikishe kwa Familia ya Mungu nchini Nigeria pamoja na wote wanaoteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ufufuo wa Yesu kristo uwe kichocheo cha: toba, wongofu, maridhiano na amani kwa watu wote wa Nigeria! Na mwisho kabisa amewakabidhi wananchi wote wa Nigeria chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria, Malkia wa Afrika. Na amewaomba kumkumbuka pia katika sala na sadaka yao.
All the contents on this site are copyrighted ©. |