2015-03-16 11:31:00

Simameni kidete kutangaza Injili ya Uhai


Mama Kanisa tarehe 25 Machi ya kila Mwaka anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari na Malaika Gabrieli kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, Siku ambayo Kanisa sehemu mbali mbali za dunia linaadhimisha Siku ya Injili ya Uhai, kwa kujikita katika mchakato unaopania kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hii ni changamoto ya kuondokana na utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba na kifo laini au Eutanasia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaiadhimisha Siku kuu kwa kusimama kidete kutetea zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, maadhimisho haya kwa Mwaka 2015 yanaongozwa na kauli mbiu “Kuna maisha tele katika kila maisha”. Huu ni mwaliko wa kuwalinda, kuwatunza na kuwatetea wanyonge, wazee na wagonjwa ambao wamekuwa ni wahanga wanaowindwa kwa udi na uvumba na utamaduni wa kifo kutokana na utamaduni wa kifo usioheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai linakumbusha kwamba, maisha ya binadamu awaye yote yana thamani kubwa kwani mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, hana mbadala. Binadamu ni kiumbe jamii anayefikia utimilifu wa maisha yake kwa kushirikiana, kujadiliana na kupendana na wengine, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo dhidi ya tabia ya ubinafsi, uchoyo na upweke hasi unaoendelea kusababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu wengi.

Utimilifu wa maisha ya mwanadamu unafikiwa kwa kusaidiwa na wengine wanasema Maaskofu kutoka Hispania, kumbe, kila mwanadamu ni zawadi kwa jirani yake. Jamii hawezi kujenga na kuimarika kwa kuwatenga na kuwaondoa maskini na wanyonge kwa kuthamini kwamba, wao wako hapa duniani kwa bahati mbaya na wala si sehemu ya mpango wa Mungu. Hapa, Jamii inashindwa kutambua thamani ya maisha na utu wa mwanadamu.

Walemavu, wagonjwa na maskini ni mashujaa wa maisha, watu wenye ujasiri na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika undani wa mwanadamu, kwa kuthamini ile sura na mfano wa Mungu katika maisha yao. Familia ambazo zina walemavu, mara nyingi zina mwelekeo tofauti wa maisha, kwani watoto wao wenye ulemavu wanakuwa kweli ni chemchemi ya: imani, furaha na matumaini yanayowasaidia wengine kuona umuhimu wa zawadi ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hisania linapenda kutoa mwaliko kwa Serikali kushirikiana na Kanisa pamoja na wadau mbali mbali kulinda na kutetea Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, ili kujenga na kuimarisha ulimwengu unaojikita katika utu na heshima ya binadamu. Ni mwaliko wa kuhudumia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuwashirikisha wote pasi na kuwatena wala kuwabagua kutokana na kasoro katika miili yao. Wadau mbali mbali wanapaswa kutekeleza dhamana hii kwa ujasiri na moyo mkuu ili kuenzi Injili ya Uhai na kukata katu katu utamaduni wa kifo unaoungwa mkono hata wakati mwingine na sheria, sera na mikakati ya maendeleo inayoshindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.