2015-03-16 09:37:00

Maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu


Katika Maadhimisho ya miaka miwili, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, Ijumaa tarehe 13 Machi 2015, wakati wa Ibada ya Toba, ametangaza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, utakaozinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2015 katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na kufungwa rasmi hapo tarehe 20 Novemba 2016 katika maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu.

 

Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Ijumaa na Jumamosi tarehe 13 na 14 Machi 2015: katika kipindi cha saa 24 waamini sehemu mbali mbali za dunia wamekesha na kusali; wametafakari na kuabudu Ekaristi Takatifu; wametubu na kuungama dhambi zao, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

 

Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu utazinduliwa rasmi kama sehemu ya kumbu kumbu ya kuhitimishwa rasmi kwa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kunako mwaka 1965, changamoto kwa Mama Kanisa kuendeleza mageuzi yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

 

Katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, masomo yatakayotumika ni kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka anayetambulikana kuwa ni Mwinjili wa huruma ya Mungu kama anavyosimulia kuhusu: Kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na Baba mwenye huruma. Tamko rasmi la Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu litatolewa tarehe 12 Aprili 2015 wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

 

kadiri ya Mapokeo, Jubilee ilikuwa inaadhimishwa kila baada ya miaka hamsini na waamini walikuwa wanalika kutenda mema na kuzingatia haki. Baba Mtakatifu Bonifasi wa nane kunako mwaka 1300 alianzisha rasmi maadhimisho ya Jubilee ambayo yangefanyika ndani ya Kanisa kila baada ya miaka 100. Kunako mwaka 1475, ili kutoa nafasi walau kwa kila kizazi kuadhimisha Jubilee, ikaamriwa kwamba, Jubilee iadhimishwe walau kila baada ya miaka 25 kama kumbu kumbu ya maadhimisho ya tukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.

 

Hadi wakati huu kuna Jubilee 26 ambazo zimekwisha adhimishwa na Mama Kanisa. Mara ya mwisho, Kanisa limeadhimisha Jubilee kuu ya Ukristo kunako Mwaka 2000. Jubilee maalum zilizowahi kuadhimishwa na Mama Kanisa ni hapo Mwaka 1933 uliotangazwa na Papa Pio wa kumi na moja ili kuadhimisha Jubilee ya miaka 1900 ya Ukombozi; Jubilee ya Mwaka 1983 iliyotangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 1950 ya Ukombozi.

 

Jubilee ni kipindi cha kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya toba na msamaha wa dhambi unaowawezesha waamini kupata rehema kamili na rehema ya muda. Ni mwaka unaowachangamotisha Wakristo kumwilisha imani yao katika matendo kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

 

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, unamweka Mwenyezi Mungu kuwa ni kiini cha maadhimisho haya. Baba Mtakatifu anatarajiwa kufungua Lango kuu la Jubilee linalofunguliwa tu wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya Kanisa na waamini wanapita langoni hapo kuomba rehema na neema katika hija ya maisha yao, wakati mwingine wote, lango hufungwa. Makanisa makuu yaliyoko Jimbo kuu la Roma yatatumika pia kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu.

 

Itakumbukwa kwamba, tema ya huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko anayependa kumwonesha Yesu aliyemwangalia Mathayo mtoza ushuru kwa jicho la huruma, akamwita naye akaacha yote na kuanza kumfuasa na leo hii ni mtangazaji mahiri wa huruma ya Mungu kwa njia ya Injili yake. Huruma ya Mungu isaidie kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kwa kujikita katika mshikamano wa upendo, haki na udugu.

 

Ni mwaliko kwa waamini walei kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili, kwa kugeuza familia, parokia na majimbo kuwa ni visiwa vya upendo dhidi ya bahari ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya binadamu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.