2015-03-16 10:00:00

Kanisa ni mtetezi wa wanyonge na maskini


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Bielorussia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Machi, 2015: ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa makazi ya Ubalozi wa Vatican nchini humo, amezungumza na viongozi wakuu wa nchi,  Baraza la Maaskofu Katoliki Bielorussia pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Familia ya Mungu nchini humo.

Kardinali Parolin wakati wa kubariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa Vatican mjini Minsk, Ijumaa tarehe 13 Machi 2015,  alibainisha kwamba, diplomasia ya Vatican inapenda kujika zaidi katika utetezi wa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa ndio akina Abeli wa nyakati hizi, ambao kilio chao cha damu hakijasikilizwa na wengi.

Ameadhimisha pia kumbu kumbu ya miaka miwili tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kwa kuonesha mshikamano wa Kanisa na wananchi wa Bielorussia katika shida na mahangaiko yao, ili kuwajengea tena imani na matumaini kwa njia ya mshikamano wa kidugu. Lengo ni kuwa na amani, ustawi na maendeleo kwa ajili ya wengi kwa kushikamana na Vatican, kwa ajili ya huduma kwa utu na heshima ya binadamu.

Uwekaji wa jiwe na msingi kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa Vatican, kuna maanisha mchakato wa kuwaimarisha Wakatoliki billioni moja na millioni mia mbili wanaoongozwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wawakilishi wake walioenea sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni sauti ya kinabii na kimaadili kwa ajili ya Familia ya Mungu. Bado kuna maelfu ya damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia, ndiyo maana Vatican itaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima; uhuru na haki msingi za binadamu.

Kanisa litaendelea kuwasaidia kwa hali na mali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na kukazia misingi ya haki na amani. Demokrasia ya kweli inapatikana kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuaminiana na wala si kwa njia ya kumwondosha mwingine katika mchakato wa demokrasia.

Kardinali Pietro Parolin, Jumamosi tarehe 14 Machi 2015 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Bielorussia, kwa kuwashukuru na kuwapongeza Maaskofu kwa mwamko na ari waliyo nayo katika maisha na utume wa Kanisa, jambo linaonesha pia ongezeko la Wakatoliki nchini humo. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kuwaimarisha waamini: kiroho, kimwili, kiutu na kimaadili, ili waweze kuwa tayari kumshuhudia Kristo na Kanisa lake kwa njia ya imani tendaji.

Hiki si kipindi cha Wakleri na Watawa kubweteka na kudhani kwamba kazi imekwisha, bali ni mwanzo wa kuimarisha mafanikio yaliyokwisha kupatikana kwa kujikita katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini waonjeshwe uhuru unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, kwa kuwa na matumizi bora ya mali na rasilimali za Kanisa, kwani hizi ni kwa ajili ya shughuli za Uinjilishaji na wala si mali ya mtu binafsi.

Majimbo na Parokia zinatakiwa kuwa na Baraza la Uchumi, ili kupanga, kuratibu na kupima matokeo ya mikakati ya maendeleo kiroho na kimwili anasema Kardinali Pietro Parolin. Waamini walei washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wahakikishe kwamba, wanatoa majiundo awali na endelevu kwa vijana wa kizazi kipya, ili kutambua na kuthamini wajibu wao kwa jamii na Kanisa katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.