2015-03-16 11:18:00

Jubilee ya huruma ya Mungu ilete mabadiliko mioyoni mwa watu


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anabainisha kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu ni sehemu ya mikakati ya kichungaji iliyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Evangelii gaudium, kwa kulitaka Kanisa kutoka na kuwaendea Watu wa Mataifa, ili kuwatangazia Injili ya Furaha inayojikita katika huruma ya Mungu.

Ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao walioupokea katika Sakramenti ya Ubatizo, unaowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo; utume unaowasukuma kuwaendelea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwashirikisha imani inayomwilishwa katika matendo.

Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; fursa makini ya kusali na kulitafakari Neno la Mungu; muda wa kufanya hija katika maeneo matakatifu ili kujipatia rehema na neema katika safari ya maisha ya kiroho, katika kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu tangu mwanzo wa utume wake aliwaambia waamini kwamba, huruma ya Mungu inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu, mwaliko ni kuipokea na kuifanyia kazi katika uhalisia wa maisha anasema Askofu mkuu Rino Fisichella. Ndiyo maana Baba Mtakatifu ameutangaza Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Upatanisho, mahali ambapo mwamini aliyejiandaa kikamilifu anaweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Hapa Mwenyezi Mungu anajitambulisha kuwa ni Mungu anayependa na kusamehe na kwamba, kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kupiga magoti mbele ya kiti cha huruma ya Mungu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kwani Mwenyezi Mungu kamwe, hachoki kumpenda, kumhurumia na kumsamehe mwanadamu wakati wote anapomkimbilia kwa moyo wa toba na majuto. Waamini wengi kwa sasa wanaanza kugundua tena umuhimu wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Askofu mkuu Rino Fisichella anasema, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho ni mwanzo wa hija ya maisha ya kiroho inayojikita katika upendo na mshikamano wa kweli. Waamini wanaokutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao, wanapaswa kumtambua pia kati ya ndugu zake wote, lakini zaidi miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Matendo ya huruma ni mambo msingi katika maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu yatazinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2015, kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipokwa wanafunga rasmi maadhimisho ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko kwa kufungua tena lango hili, anataka kulialika Kanisa, kumwilisha tena zile juhudi za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walizoonesha kwa kipindi cha miaka minne, ili kuwatangazia tena Watu wa Mataifa, huruma ya Mungu inayokoa na kuponya, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.

Walimwengu wanasubiri kwa hamu kuona jinsi ambavyo huruma ya Mungu inawagusa katika undani wa maisha yao anasema Askofu mkuu Rino Fisichella. Huruma ya Mungu ndiyo changamoto kubwa ambayo imetolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika kipindi chote hiki cha miaka hamsini ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, Kanisa linataka kujiimarisha katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.