2015-03-16 10:32:00

Dumisheni majadiliano ya kidini


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini anaialika Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba inajitahidi kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kuimarisha amani, umoja, mshikamano na maridhiano kati ya watu bila ya kubeza wala kukashifu dini za watu wengine. Watu wajenge utamaduni wa kuthaminiana na kuheshimiana hata katika tofauti zao mbali mbali kwa kutambua kwamba, ni utajiri mkubwa katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa wengi na kamwe tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha chokochoko na kinzani ambazo mara nyingi zinapelekea maafa makubwa kwa watu.

Kardinali Tauran ameyasema haya, mwishoni mwa juma wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 110 tangu Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe ilipokumbatia imani ya Kikristo, huko Korhogo. Wakristo wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kimaadili kwa majirani yao, kama chachu ya kuyatakatifuza malimwengu. Mchakato huu unawezekana pale ambapo kuna: haki, amani na utulivu na kwamba, watu wanaweza kukumbatia kweli za kiimani pasi na bughuza za maisha.

Kardinali Tauran anasema, kiini cha dini yoyote ile duniani ni: umoja, udugu na amani, changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kuwa kweli ni wajenzi na madaraja ya amani, upendo na mshikamano, kwa kuheshimiana na kusaidiana ili kukua na hatimaye, kufikia ukomavu katika medani mbali mbali za maisha. Kuna hitaji moyo wa uvumilivu na sadaka ili waamini wa dini mbali mbali waliokuwa hawaaminiani kuanza kufanya hija ya pamoja katika maisha yao. Lakini, ikumbukwe kwamba, tofauti zao ni utajiri mkubwa unaopaswa kudumishwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Waamini wajifunze kuvumiliana, kupendana, kufahamiana na kupokeana jinsi walivyo.

Kardinali Tauran katika hija yake ya kichungaji nchini Pwani ya Pembe, ametembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Ambrose pamoja na kutembelea Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Magharibi, UCAO. Hapa amekazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusikilizana na kuheshimiana katika ukweli, wema na utakatifu wa maisha ambao Mwenyezi Mungu ameuweka mbele ya waja wake.

Kardinali Tauran anasema kwamba, amani ni changamoto endelevu kwa Mama Kanisa pamoja na wadau mbali mbali, kwani kuna uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, licha ya Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kukazia haki msingi za binadamu. Pwani ya Pembe ni nchi ambayo pia imepitia kurasa chungu za maisha, zinazohitaji kugangwa na kuponywa kwa kuzingatia ukweli, msamaha na upatanisho wa kitaifa. Huu ni mchango mkubwa ambao unaendelea kutekelezwa na Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.