2015-03-16 09:44:00

Changamoto za maisha nchini Nigeria


Mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria, hali ya amani na usalama,  idadi kubwa ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi pamoja na changamoto za uchaguzi mkuu ni kati ya mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria. Haya yamebainishwa hivi karibuni katika mahojiano maalum na Shirika la Kipapa kwa ajili ya msaada kwa Makanisa hitaji.

Viongozi wa Kanisa wanatakiwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume wao wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika: sheria, kanuni na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuisaidia Familia ya Mungu nchini Nigeria kuweza kufanya uchaguzi unaowajibisha, ili hatimaye, kuwapata viongozi watakaosimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi.

Askofu mkuu Kaigama anasema, shutuma kwamba, Kanisa limepokea “vigunia vya fedha” kwa ajili ya kusaidia kampeni ili Rais Goodluck Jonathan aweze kushinda uchaguzi mkuu ni uvumi usiokuwa na ukweli wowote. Baraza la Maaskofu Katoliki limebahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wote wanaowania madaraka katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Kanisa limewaambia viongozi wote hawa kwamba, watu wanataka kupata viongozi wazalendo, wakweli, waaminifu, wachamungu na waadilifu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Nigeria. Umefika wakati kwa viongozi wa Nigeria kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wananchi badala ya kujitafuta wenyewe na kwa ajili ya masilhai yao binafsi.

Taifa linawaihtaji viongozi ambao wanaweza kutumia rasilimali ya nchi vyema ili kupambana na umaskini, ukosefu wa ajira pamoja na kuwahakikishia wananchi usalama wa maisha na mali zao.

Kanisa kwa upande wake, linaendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kuwajengea wananchi utamaduni wa kujikita katika ukweli, haki, msamaha na upatanisho wa kitaifa, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini. Dini isiwe ni chanzo cha vita, vurugu na kinzani za kijamii, bali chombo cha umoja, upendo na mshikamano wa dhati.

Serikali ya Nigeria inabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni moja ambao hawana makazi ya kudumu kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram, Kaskazini mwa Nigeria. Kuna wakimbizi 36, 000 wanaohudumiwa nchini Cameroon. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali wanaendelea kuwahudumia wakimbizi hawa kwa matumaini kwamba, hatimaye, wataweza kurejea tena nchini Nigeria ili kuendelea na maisha yao ya kila siku. Askofu mkuu Kaigama anabainisha kwamba, Serikali kwa miaka mingi imelifumbia tatizo la misimamo mikali ya kidini, bila kulishughulikia kikamilifu na matokeo yake ni mashambulizi y amara kwa mara yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Inasikitisha kuona kwamba, Serikali ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vitendea kazi, inashindwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram. Wakati huu wa kampeni ya uchaguzi mkuu, kila Rais mtarajiwa anajinadi kwa kusema kwamba, tayari ana dawa ambayo kwa sasa inachemka, akingia tu madarakani, atawawaonesha cha mtema kuni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.