2015-03-14 15:25:00

Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu


Sakramenti ya Upatanisho inamwezesha mwamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu anayewasamehe wale wote wanaotubu dhambi zao kwa moyo wa unyenyekevu. Katika historia ya maisha ya mwanadamu, Mwenyezi Mungu ameendelea kumwonesha na kumwonjesha huruma na kwamba, neema yake inamwezesha mwamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

 

Ni mwaliko wa kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu pasi na woga kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu atawapokea, atawasikiliza na hatimaye, kuwasamehe dhambi zao. Mwamini anapotoka kwenye kiti cha maungamo anajaliwa tena nguvu ya maisha mapya inayobubujika kutoka katika imani na kuwa watu wapya zaidi. Toba na wongofu wa ndani ni hija ya matumaini na faraja yanayotoka kwa Kristo, hakimu mwenye haki na mwingi wa huruma na mapendo.

 

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 13 Machi 2015 alipokuwa anaongoza Ibada ya Toba, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baada ya kuungama dhambi zake, naye aliketi kwenye kiti cha huruma ya Mungu ili kuwaungamisha waamini waliokuwa wamejiandaa Kanisani hapo. Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameshiriki Ibada ya toba, sala, tafakari sanjari na kuabudu Ekaristi Takatifu, kama sehemu ya mchakato wa kukimbilia huruma ya Mungu wakati huu wa Kwaresima.

 

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema kwamba, upendo na huruma ni tunu zinazoambatana na kwamba, Yesu ambaye ni mwingi wa huruma, anasamehe pasi na kuhukumu kama ilivyotokea kwa yule mwanamke mdhambi aliyempaka Yesu mafuta yenye harufu nzuri, kiasi cha kuzua minong'ono miongoni mwa watu waliokuwa wamekaribishwa nyumbani kwa Petro. Mwanamke alitubu na kuungama dhambi zake, akaonja huruma na upendo wa Mungu unaovuka haki n akukumbatia ukweli.

 

Baba Mtakatifu anasema, Yesu anawachangamotisha waamini  kuzama katika undani wa maisha yao na kamwe wasibaki wanaelea katika ombwe, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni nyumba ya huruma ya Mungu inayowapokea na kuwakumbatia wote; watakatifu na wadhambi wanaotambua mapungufu yao na wako tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Kwa njia ya upendo, Yesu anaponya na kuganya mioyo iliyopondeka na kuvunjika kutoka na dhambi.

 

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa halina budi kutekeleza dhamana wito wake wa kuwa ni shuhuda wa huruma ya Mungu, hija inayojikita katika toba na wongofu wa ndani. Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu anasema, ameamua kutangaza Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; ambamo waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kumwilisha ujumbe wa Injili kwa kuwa ni watu wenye huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma.

 

Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, utafunguliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2015, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na kufungwa rasmi, tarehe 20 Novemba 2016 katika Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Maadhimisho ya Mwaka huu yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kama hatua ya hija ya Mama Kanisa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Huruma ya Mungu.

 

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna umati mkubwa wa Familia ya Mungu unaohitaji kuonja huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, wao ni wadhambi, kumbe Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu unapania kuwaonjesha na hatimaye, watu wenyewe waweze kuonjeshana huruma hiyo kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hachoki kuhurumia na kusamehe, mwaliko kwa waamini kuongeza bidii ya kukimbilia huruma ya Mungu.

 

Baba Mtakatifu Francisko anaukabidhi Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu chini ya usimamizi na maongozi ya Bikira Maria Mama wa huruma. Hija ya toba na wongofu wa ndani katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu utawawezesha waamini watakaokuwa wamejiandaa barabara kupokea rehema kamili na huruma ya Mungu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.