2015-03-06 14:30:00

Tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2015


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mstaafu Renato Corti wa Jimbo Katoliki Novara, Italia, kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba itakayotumika Ijumaa kuu, tarehe 3 Aprili 2015 kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma. Tafakari hii itafuata Tafakari ya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, yaani kutakuwepo na Vituo 14 vya Njia ya Msalaba.

Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, inayopaswa kutangazwa sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa na kwa njia hii, watu wanaonja neema na baraka; upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mama Kanisa anawakumbusha walimwengu kwamba, Yesu alijitoa mwenyewe kwa Baba yake wa Mbinguni kwa ajili ya dhambi za binadamu, akajisadaka ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambi na mauti. Yesu ndiye yule Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia anayependa kuwaonjesha walimwengu mapeno ya Baba yake kwa njia ya utii kamili kama kielelezo cha mapendo upeo.

Msalaba ni ngazi ya kuwafikisha waamini mbinguni. Ni ishara ya mapendo, neema sala, msamaha na matumaini, ndiyo maana Wakristo wanaona fahari kubwa sana juu ya Msalaba wa Yesu Kristo, Mti ambao wokovu wa binadamu umetundikwa juu yake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kulitafakari Fumbo la Msalaba, kuuabudu, kuuheshimu na kuutukuza kwa imani, mapendo na matumaini makubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.