2015-03-06 11:52:00

Mchango wa Papa Paulo VI kwa ustawi wa Kanisa Barani Afrika


Mwenyeheri Paulo VI ni kati ya Mababa Watakatifu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika harakati za uhuru kwa nchi nyingi Barani Afrika, tangu alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia. Ni kiongozi aliyeihamasisha Familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika mchakato wa utamadunisho ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya watu wengi Barani Afrika.

Tunu msingi za Kiinjili zilikuwa na dhamana ya kusafisha na kuboresha mila na tamaduni zilizokuwa zinasigana na Injili sanjari na kukumbatia pia mila na tamaduni njema kutoka Barani Afrika kama sehemu ya mchakato wa kulitajirisha Bara la Afrika katika maisha na utume wa Kanisa. Mwenyeheri Paulo VI alitambua na kuthamini utu na heshima ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

Haya ni kati ya mambo ambayo yameibuliwa kwenye Kongamano la Kimataifa linaloendeshwa na Radio Vatican, ili kuangalia mchango wa Mwenyeheri Paulo VI katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika mintarafu utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa.

Wajumbe wa kongamano hili wanabainisha kwamba, maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaliyokwenda sanjari na harakati za kupigania uhuru kwa nchi nyingi Barani Afrika, kilikuwa kweli ni kipindi cha matumaini na maendeleo ya kweli. Ni wakati huu, matumaini haya yalipoingia kasoro kutokana na vita baridi kati ya Marekani na Urussi, Papa Paulo VI kwa ujasiri mkubwa akaamua kuandika Waraka wa kichungaji kuhusu: Amani duniani “Pacem in Terris, akikazia: utu na heshima ya binadamu; haki na amani; pamoja na maendeleo endelevu.

Wajumbe pia wanatambua mchango mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa mara ya kwanza katika historia, Kanisa Barani Afrika likaanza kuchomoza kama nyota ya asubuhi, hata kama Ukristo ulikwishaingia Barani Afrika tangu  Karne ya pili huko Misri na Karne ya IV nchini Ethiopia, hiki ni kipindi ambacho hata Wamissionari walikuwa hawapata wazo la kwenda Barani Afrika ili kushiriki kazi ya Uinjilishaji kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto VI, aliyeihamasisha Familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika utajiri na urithi mkubwa unaofumbatwa katika tamaduni zake.

Mwenyeheri Paulo VI alipenda kukazia masuala ya uhuru, demokrasia ya kweli, haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Alikuwa na ujasiri wa kuwasikiliza wapigania uhuru ambao kwa mataifa mwengi walionekana kuwa ni wasaliti na majasusi, ugaidi ulikuwa haujaanza kupamba moto kwa wakati ule.

Washiriki wa kongamano linaloangalia mchango wa Mwenyeheri Paulo VI kwa Bara la Afrika wanasema, kuna haja kwa wananchi Barani Afrika kukazia na kujikita katika tunu msingi zilizopiganiwa na waasisi wa Mataifa ya Kiafrika, kwa kujiwekea pia sera na mikakati kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi Barani Afrika. Viongozi wa Bara la Afrika wawe ni vikolezo vya maendeleo kwa wananchi wake, ili kuweza kulikwamua Bara la Afrika katika mawazo mgando, vita, ukabila, udini na ubinafsi; mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa kama ndio mtindo wa maisha Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.