Baraza la Kipapa la haki na amani linabainisha kwamba, Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Amani na utulivu duniani vitaendelea kuwa ni ndoto ya mchana ikiwa kama bado kuna umati mkubwa wa watu unaoogelea katika lindi la njaa na umaskini.
Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yanayobainishwa katika Waraka wa Dunia na Chakula, ulioandikiwa hivi karibuni na Baraza la Kipapa la haki na amani, kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika kujibu changamoto za ukosefu wa amani duniani. Dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa binadamu wote, lakini shida kubwa hapa ni utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuzalisha chakula bora na kinachotosheleza mahitaji ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira na vyanzo vya maji. Mageuzi ya sera na mikakati ya shughuli za kilimo hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu badala ya mwelekeo wa sasa wa kutaka kupata faida kubwa pamoja na kuwapokonya wakulima wadogo wadogo maeneo ya ardhi kwa kisingizio cha kilimo cha kisasa.
Baraza la Kipapa la haki na amani linabainisha kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa yamekuwa ni dira na mwongozo unaofafanua masuala mbali mbali mintarafu taalimungu, kanuni maadili na mikakati ya shughuli za kichungaji. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Baraza la Kipapa la haki na amani limechapisha Nyaraka kuu nne. Kunako mwaka 2011 lilichapisha Waraka unaozungumzia mageuzi katika mfumo wa fedha na mashirika ya fedha kimataifa.
Kunako mwaka 2012 Baraza likachapisha Waraka kuhusu maji ni uhai na kamwe hayawezi kugeuzwa kuwa ni sawa na bidhaa nyingine. Mwaka 2012, Baraza lilichapisha waraka kuhusu wito wa viongozi wa makampuni. Mwaka 2013, Baraza la Kipapa likachapisha Waraka kuhusu Nishati mintarafu haki na amani. Na mwaka 2015 Waraka kuhusu; Dunia na Chakula. Nyaraka hizi zote zinategemeana na kukamilishana, linasema Baraza la Kipapa la haki na amani na zimeandikwa kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kuwasaidia wadau mbali mbali kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anaandaa Waraka wa Kichungaji kuhusu Mazingira, kwa kutambua kwamba, hata Wakristo wanayo dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira. Huu ni mwelekeo wa imani katika masuala ya kisiasa, ili kuhakikisha kwamba, wanazingatia upendo na ukweli ulioletwa na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Hii pia ni changamoto ya Uinjilishaji mpya, unaowataka Wakristo kushuhudia imani yao kwa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya sasa na yale ya kizazi kijacho.
Mwaliko ni kulinda Injili ya Uhai kwa kutunza ekolojia ya binadamu, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uhai, utu na heshima ya binadamu. Baraza la Kipapa la haki na amani linabainisha kwamba, ekolojia ya mazingira na binadamu ni sawa na chanda na pete, kwani mambo haya mawili yanategemeana na kukamilishana. Ni wajibu wa Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kutunza mazingira hata kabla ya kuhamasishwa na vyama vya kisiasa au watetezi wa mazingira duniani.
Tangu mwanzo, Mababa wa Kanisa na Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume yamekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira, kwani huu ni wito wao unaobubujika kutoka katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa maneno mengine, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.
Wadau wengi wanasubiri kwa hamu Waraka wa kitume unaoendelea kuandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mazingira na maendeleo endelevu ya binadamu; kwa kuzingatia: uzuri, wema na ukweli kuhusu kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza, kwani mazingira ni maskani ya wote; kwa watu wa kizazi cha sasa na kile kijacho.
Ni Waraka ambao utajielekeza zaidi na zaidi katika kudumisha mshikamano, haki na mafao ya wengi. Hapa ekolojia ya binadamu inapewa kipeumbele cha kwanza, kwa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa ujasiri, mshikamano, weledi na ugunduzi, kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu ya mchakato wa kazi ya Ukombozi iliyofanywa na Yesu Kristo. Matunda ya Waraka huu wa kitume, yatapatikana kwa wakati wake.
Leo hii kuna mengi ambayo watu wanaendelea kujifunza kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume: Upendo katika Ukweli; Caritas in veritate. Binadamu na utu wake ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si fedha na faida kubwa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |