Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 7 Machi 1967 kwa mara ya kwanza aliadhimisha Fumbo
la Ekaristi Takatifu kwa lugha ya Kiitalia, kwenye Parokia ya Watakatifu wote, Jimbo
kuu la Roma, kama sehemu ya mchakato wa utekekelezaji wa mabadiliko makubwa yaliyofanywa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa,
ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa kikamilifu na mwanadamu kutakatifuzwa katika maisha
yake.
Huu ukawa ni mwanzo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu katika
lugha mbali mbali, kikiwemo Kiswahili ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu
katika Mafumbo ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamwimbia Mwenyezi
Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani leo hii kuna ushiriki mkubwa wa waamini katika
maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ikilinganishwa na wakati ule, Ibada ya Misa Takatifu
ilipokuwa ikiadhimishwa kwa lugha ya Kilatini.
Huu ni utambuzi wa shughuli
za kichungaji ulioliwezesha Kanisa kuona umuhimu wa kuisaidia Familia ya Mungu kufahamu
na hatimaye, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, mchango
mkubwa wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Liturujia ya Kanisa. Hivi
ndivyo anavyofafanua Padre Giuseppe Midili, Mkurugenzi wa Idara ya Liturujia, Jimbo
kuu la Roma, wakati huu, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Familia
ya Mungu nchini Italia na hatimaye, sehemu mbali mbali za dunia, ilipoanza maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa lugha ya Kiitalia.
Hii ni changamoto inayomtaka
mwamini kutambua kwamba, adhimisho la Liturujia ni mchakato wa majadiliano ya kina
kati ya Mwenyezi Mungu na mja wake, jambo lililosisitiziwa na Mwenyeheri Paulo VI.
Waamini wanapaswa kusali na kuzungumza na Mwenyezi Mungu katika lugha wanayoifahamu,
huu ukawa ni mwanzo pia wa utamadunisho wa Injili ya Kristo katika tamaduni mbali
mbali duniani. Ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa
unapata chimbuko lake msingi katika Sakramenti ya Ubatizo na kigezo muhimu katika
mageuzi yaliyoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Baada ya
changamoto hii, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali yalianza kuunda kamati
za kuangalia uwezekano wa kutekeleza taalimungu iliyokuwa imefafanuliwa na Mwenyeheri
Paulo VI, ili iweze kutekelezwa katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Kanuni
za mabadiliko ambazo zilipaswa kuzingatiwa katika kuandika vitabu vya Liturujia, zilibainishwa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wake kuhusu Mabadiliko
ya Liturujia, yaani “Sacrosanctum concilium”.
Hadi leo hii, Kanisa bado linaendelea
kutekeleza changamoto za mabadiliko katika Liturujia zilizoletwa na Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican, ndiyo maana hivi karibuni kumekuwepo na tafsiri mpya ya vitabu
vya Liturujia, katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili kuwawezesha waamini kukutana
na kuzungumza na Kristo pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini wanafanikiwa kumpeleka
Kristo kwa Watu wa Mataifa kadiri ya lugha na tamaduni zao. Lengo ni kumwilisha imani
katika wongofu wa ndani; kwa kutumia lugha na alama ambazo zinaeleweka vyema zaidi
na Familia ya Mungu katika taifa husika.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka
wake wa Kitume, Injili ya Furaha anabainisha kwamba, Kanisa linainjilisha na kuinjilishwa
kwa njia ya ubora wa lugha inayotumiwa, ili kuwawezesha waamini kwa njia ya maadhimisho
ya Liturujia ya Kanisa, kutambua chemchemi ya maisha ya Kikristo pamoja na kushiriki
kikamilifu katika adhimisho la Fumbo la Pasaka. Waamini wanachangamotishwa na Mama
Kanisa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kamwe wasiwe
ni wasikilizaji au watazamaji tu wa kile kinachoadhimishwa na Padre Altareni.
Lugha
ya Kilatini bado inaendelea kutumiwa na Mama Kanisa kama lugha ya Kanisa, ndiyo maana
katika maisha na utume wake, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliwahamasisha waamini
kujifunza na kuipenda lugha ya Kilatini, kwani ni muhimu sana katika maisha na utume
wa Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.