2015-03-02 15:03:36

Ukatili unaoendelea Syria na Iraq -hauvumiliki


Baba Mtakatifu Francisco, Jumapili iliyopita ambamo Mama Kanisa aliadhimisha tukio la Yesu kubadilika sura, nyakati za adhuhuri, akihutubia maelfu ya mahujaji na wageni katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alielekeza mawazo ya watu huko Syria na Iraki , akisema ni vigumu kupuuza mateso na ukatili unaofanyika Syria na Iraq. Ni ukatili usiovumilika. Na pia alitoa wito wa kukumbuka katika sala watu wa Venezuela, wakati huu wanapopita katika kipindi kigumu cha mivutano ya kisiasa. Hotuba ya Papa iligusia matukio mengi yanayoendelea kusikika hapa na pal yenye vurugu, utekaji nyara na unyanyasaji dhidi ya Wakristo na makundi mengine.

Baba Mtakatifu aliwahakikishia wote waliokumbwa na mateso haya kwamba, kiroho yuko pamoja nao, daima akitolea sala zake , akiomba ukatili huu usioweza kuvumilika, usitishwe haraka iwezekanavyo. Papa alieleza na kutaja kwamba pia o imekuwa nia yake kuu wakati wa mafungo yake ya kiroho ya wiki iliyopita, aliyoyafanya akiwa pamoja na wakuu wa Idara za Curia ya Roma. Mafumngo aliyo kamilisha siku ya Ijumaa iliyopita kwa ibada ya Misa. Katika wiki hilo, Papa alitoa wito kwa kila mtu, kulingana na uwezo wao, kushiriki kwa namna moja au nyingine kusaidia kupunguza mateso ya wale walio katika mateso na taabu nyingi , kwa sababu ya kukiri imani yao.
Aidha Papa alielekeza mawazo yake Venezuela, ambako katika siku hizi , taifa limeingia katika msukosuko mpya wa upinzani mkali dhidi ya serikali, ambako katika maandamano mapya dhidi ya serikali, kijana wa miaka 14 alipoteza maisha wakati wa kukabiliana na polisi. Papa alitoa ombi la kuwakumbuka waathirika ghasia hizo na hasa kijana huyo aliyepoteza maisha mjini San Cristobal.
Papa amekemea kila aina ya wazo linalotaka kujenga ghasia na machafuko yasiyoheshimu utu wa mtu na utakatifu wa maisha ya binadamu na kuhimiza kutembea katika njia za pamoja kwa amani, kwa manufaa ya nchi, hasa kufungua nafasi kwa ajili ya mikutano na mazungumzo ya dhati yenye kujenga nchi . Papa alieleza na kuiweka nchi hiyo pendwa chini ya maombezi kimama ya Mama yetu ya Coromoto.
Na akirejea kwamba, hii ilikuwa ni Jumapili ya pili ya Kwaresima, alisema , Kanisa linatuonyesha lengo la hija ya uongofu kwamba ni kushiriki katika utukufu wa Kristo. Papa alieleza hivyo akilenga katika somo la Injili , ambamo Yesu alibadilika sura mbele ya wanafunzi wake, Petro, Yakobo na Yohane. Alisema fundisho kwetu ni kuisikiliza sauti ya Yesu Mkombozi na kumfuata.

Aliongeza, kumsikiliza Kristo kwa kweli, kunaonyesha mantiki ya Siri ya fumbo lake la Pasaka, kwamba ni kutembea pamoja naye katika njia yake ya maisha yenye zawadi ya upendo kwa wengine, katika unyenyekevu wa utii na mapenzi ya Mungu. Hiyo ina maana ya kujiweka mbali na mambo ya kidunia, kwa hiari kamili. Ni lazima, kwa maneno mengine, kuwa tayari "kupoteza maisha yetu, kutoa kwa ajili ya wengine ili kwamba watu wote waokolewe na kukutana katika furaha ya milele.

Njia ya Yesu - alisema Baba Mtakatifu, daima huongoza katika furaha. Lakini pia tusisahau kwamba kutembea katika njia hii pia ni kuwa katikati ya msalaba na katika kuwa mashahidi, lakini mwisho daima huongoza katika furaha kamili. Na Yesu hadanganyi, lakini ataitimiza ahadi aliyoitoa kwa waamini wake. Kama ilivyokuwa kwa Petro, Yakobo na Yohana - Papa alihitimisha, pia sisi na tupande na Yesu katika mlima, ambako tutamwona akibadilika sura, ili tukubali ujumbe wake na kupata tafsiri yake katika maisha yetu, kwa sababu sisi pia tunaweza kubadilishwa sura kwa upendo wake Yesu. Kwa kweli upendo wa Yesu una uwezo wa kubadilisha kila jambo katika maisha yetu.








All the contents on this site are copyrighted ©.