2015-03-02 08:35:40

Mkoa wa Mbeya kugawanywa!


Serikali ya Tanzania imeyapokea maombi ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) cha Mkoa wa Mbeya yanayopendekeza mkoa huo ugawanywe na kupata mikoa miwili ya Mbeya na Songwe. Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa mkoa huo ambao una kilometa za mraba 63,000.

“Tumekwishapokea maombi ya kuugawanya mkoa wa Mbeya kwa sababu mkoa huu una eneo la kilometa za mraba 63,617 zilizogawanyika katika Wilaya 8 na Halmashauri 10. Hili ni eneo kubwa sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma maendeleo,” alisema.

Alisema kamati hiyo imeshauri mkoa huo ugawanywe katika wilaya nne nne ambapo mkoa mpya wa Songwe utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya. Wamekubaliana kuwa makao makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa chunya mmeenda mbali zaidi kwa kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya ambapo chunya itaenda Mbeya,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kwamba makao makuu ya wilaya mpya ya Songwe yatakuwa Mkwajuni. “Nimekubali maombi haya kwa sababu yatapunguza gharama za uendeshaji, na kama itashindikana kupata wilaya mpya basi itabidi tuwape Halmashauri ya Songwe,” alisema. Mkoa wa Mbeya una wilaya nane ambazo zimegawanyika katika tarafa 27, kata 262, vijiji 842 na mitaa 252. Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 2,707,410.

Akizungumzia kuhusu mpango wa maji katika wilaya hiyo, Waziri Mkuu alisema bado kuna changamoto kubwa ya kufikisha maji vijijini ambako upatikanaji wake uko kwenye asilimia 46. “Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa vitatu na mwakani tuna mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11, tunachohitaji ni fedha na usimamizi,” alisema.

Alivitaja vijiji viyakavyopata visima hivyo ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala, Isangawana, Galula, Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile, Bitimanyanga na Mapogoro.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezindua maabara tatu katika shule ya sekondari ya Saza ambazo zimejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta. Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya, Bi. Sophia Kumbuli alisema ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu sh. Milioni 268.5 vikijumuisha pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi.

“Kati ya hizo sh. Milioni 23.5 ni za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali na sh. Milioni 245 ni ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji na gesi,” alisema.

WAZIRI MKUU AWAJULIA HALI MAJERUHI WA AJALI MBEYA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewatembelea askari wa Jeshi la Polisi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kutokana na ajali waliyoipata Jumamosi wakati msafara wake ukielekea Kata ya Galula wilayani Chunya. Waziri Mkuu aliwatembelea majeruhi hao na kuwapa pole Jumapili, Machi Mosi, 2015) kabla ya kuelekea wilayani Mbozi kuendelea na ziara yake ya Mkoa wa Mbeya. Alifuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Seif Mhina.

Akizungumzia hali ya majeruhi hao, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Ismail Macha alisema, Jumamosi walipokea majeruhi tisa lakini watatu walifanyiwa uchunguzi wa afya zao na kuruhusiwa na wengine sita ilibidi wawalaze na kuwafanyia uchunguzi zaidi kutokana na hali zao zilivyokuwa. “Wengi wao walipata zaidi mshtuko ndiyo maana tukaamua kuwalaza ili tuendelee kuwapa uangalizi wa karibu… Mmoja tu ndiye amevunjika mkono wa kulia lakini wengine walipata michubuko miguuni, mikononi na usoni,” alisema.

Aliwataja waliolazwa kuwa ni Deogratius Nandi (31), Paulin Masolwa (27), Omary Hussein (24), Hamisi Haji (29) ambao wote ni wanaume. Majeruhi wa kike ni Cecilia Mussa Kabona (28) na Mwazanije Hassan (23) ambaye amevunjika mkono wa kulia. Waliopata matibabu na kuruhusiwa ni Mashaka Shabani (42), Khalifa Rashid (26) na Joel Cheja (21).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni vumbi na kokoto barabarani ambazo zilifanya gari hilo la FFU lisesereke na kupinduka. Hata hivyo, alisema mwendo mdogo wa gari hilo ulisaidia kuokoa maisha ya askari hao.

“Ajali ilitokea saa 5:30 asubuhi eneo la Chang’ombe ya Mjele. Eneo lile lina kokoto kubwa kubwa ambazo zilisababisha gari lao kuserereka na kupinduka… gari halikuwa kwenye mwendo mkali ndiyo maana askari hao wamepata majeraha madogo madogo,” alisema.

UTORO NA MIMBA ZA WANAFUNZI ZAMTIA KINYAA WAZIRI MKUU

Wakati huo huo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameendelea kukemea tabia za utoro na mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Chunya baada ya kupewa taarifa kwamba watoto 4,420 walitoroka shule na wengine 201 kupata mimba. Februari 26, mwaka huu, Waziri Mkuu aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaka na kuwakamata wale wote waliohusika na utoro na ujauzito wanafunzi na kuwafikisha mahakamani mara moja ili liwe fundisho kwa wengine baada ya kuelezwa kwamba wanafunzi 94 walipata ujauzito na wengine 645 kuacha shule kwa sababu ya utoro.

Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jumamosi, Februari 28, 2015 kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu alisema haiwezekani kuiacha hali hiyo iendelee huku watoto wa wilaya hiyo wakiharibiwa maisha kwa kukosa masomo. “Utoro kwenye shule za msingi, taarifa ya wilaya inaonyesha watoto 1,979 waliacha shule kati ya mwaka 2010 na 2014 ambao ni wastani wa watoto 395 kila mwaka na katika suala la mimba, taarifa hiyo inasema watoto 161 waliachishwa shule kwa sababu ya ujauzito,” alisema.

“Haiwezekani kabisa! Hivi akinababa kuamua kutembea na mtoto shule ya msingi ni lipi hasa unalolitaka kwake… unamwachisha shule mtoto kwa lipi hasa, hapana. Nimeshatoa agizo wahusika wakamatwe. Wa zamani tunaweza tusiwapate, lakini hawa wa mwaka jana kwa shule za msingi wako 28, RC na watendaji wako fuatilieni na muwapeleke kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza. Akichanganua takwimu za sekondari, Waziri Mkuu alisema kati ya mwaka 2010 na 2014 wanafunzi 2,251 waliacha shule kwa sababu ya utoro na wengine 40 waliachishwa kwa sababu ya ujauzito.

“Ninawasishi wazazi na uongozi wa wilaya na mkoa tufanye jitihada kuhakikisha jambo hili linakomeshwa mara moja. Huwezi kununua madaftari an kumlipia ada tu halafu usitake kuona mwanao anamaliza shule. Kila mzazi ana jukumu la kuhakikisha mtoto wake anamaliza shule ili awe na maisha bora hapo baadaye,” alisema Waziri Mkuu. “Nirudie kuwakumbusha wazazi kwamba mtoto wa mwenzio ni mtoto wako, huwezi kukubali maisha yaharibike hivi hivi. Tuungane pamoja kuhakikisha tunashinda vita hii,”alisisitiza.








All the contents on this site are copyrighted ©.