Serikali ya Tanzania imesema itajitahidi kuhakikisha inalipa deni lote la mahindi
yaliyonunuliwa kutoka kwa wakulima na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
ifikapo Machi 30, mwaka huu. Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika Jumapili, Machi 2, 2015 kwenye uwanja wa CCM wa Vwawa wilayani Mbozi,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imedhamiria kufuta deni lote.
“Hapa
Mbozi tulikuwa tunadaiwa sh. bilioni 21 lakini tumetoa sh. bilioni 4.5 kwa hiyo tutabakia
na deni la kama sh. bilioni 16 ambalo tunajitahidi liwe limeisha ifikapo mwishoni
mwa mwezi huu,” alisema. “Tunachoweza kuahidi kama Serikali ni kwamba, msimu huu hatutarudia
kosa la mwaka jana ingawa mtihani mkubwa tulionao ni wa kushughulika na hifadhi ya
chakula kwa kujenga vihenge (SILOS) ili hata kama kuna ziada n tusipate taabu ya kuhifadhi,”
aliongeza.
Alisema alishakwenda Poland kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete
na wao wameshakuja kuona hali halisi ilivyo. “Tumependekeza vihenge vijengwe kwenye
kanda za Mbeya, Rukwa, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha au Kilimanjaro na Shinyanga ili
iweze kuhudumia kanda ya Ziwa,” alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mbozi ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi amesema Serikali
imekwishalipa zaidi ya sh. bilioni 81 na kwamba deni lililosalia linafikia sh. bilioni
59. “Hadi mwishoni mwa mwaka jana, tulikuwa tumeshalipa sh. bilioni 51.5/- na mwaka
huu tumepata sh. bilioni 15 kutoka CRDB na hivi majuzi kuna bilioni nyingine 15 zimetoka
Hazina… Agizo la Serikali ni kwamba mahindi yote yawe yamelipwa ifikapo Machi 30,
naamini tutakamilisha,” alifafanua.
Alielezea pia tatizo la maji linaloukabili
mji wa Mbozi na vitongoji vyake na kueleza kwamba Serikali inashughulikia tatizo hilo
katika programu mbalimbali.
Mapema, akiwa katika ghala la nafaka la NFRA katika
makao makuu ya wilaya ya Mbozi, Vwawa, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kanda ya Makambako
ambayo inajumuisha vituo vya Makambako na Vwawa imezidiwa uwezo na sasa wanalazimika
kuhifadhi magunia ya mahindi nje kwa vile maghala yamejaa.
Meneja wa Kanda
hiyo wa NFRA, Bw. Abdillah Nyangasa alisema kanda hiyo ina uwezo wa kuhifadhi tani
za nafaka 34,000 ambapo kati ya hizo, tani 22,000 ni maghala ya Makambako na tani
12,000 ni maghala ya Vwawa, Mbozi.Hata hivyo, Bw. Nyangasa alisema kanda hiyo kwa
sasa kina tani za mahindi 79,496.8 zikijumuisha tani 15,738.9 za msimu uliopita licha
ya tani 63,757.8 ambazo zimenunuliwa katika msimu huu.
“Ili kukabiliana na
uhaba wa maghala, kanda yetu hulazimika kufanya hifadhi ya nje (outside storage) kwa
kutumia maturubai (tarpaulins) ili mahindi yasiharibiwe na hali ya hewa kama mvua
au jua kali,” alisema Bw. Nyangasa.