2015-03-02 13:58:27

CERNA, wahudumu wa matumaini Kaskazini mwa Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika, CERNA, limehitimisha hija yake ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican. Maaskofu hawa wamemkabidhi Baba Mtakatifu nakala ya barua ya kichungaji kwa ajili ya Familia ya Mungu Kaskazini mwa Mwafrika inayoongozwa na kauli mbiu “Watumishi wa matumaini, Kanisa Katoliki Kaskazini mwa Afrika kwa nyakati hizi”. RealAudioMP3

Barua hii imegawanyika katika ibara kuu nne zinazogusia: Mageuzi Kaskazini mwa Afrika; maendeleo ya Makanisa mahalia; utume na ushuhuda wa Makanisa haya; ufuasi kwa Bikira Maria.

Maaskofu wanabainisha kwamba, cheche za mapinduzi ya Nchi za Kiarabu, athari za myumbo wa uchumi kimataifa na ongezeko kubwa la wimbi la wahamiaji kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika ni kati ya changamoto kubwa ambazo Kanisa linakabiliana nazo huko Kaskazini mwa Afrika, kiasi hata cha kutishia mchakato wa ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Hii ni changamoto kubwa katika uhuru wa kuabudu na kwamba, mambo yote haya yanaathari kubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kaskazini. Uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu, maridhiano ndani ya jamii na tunu msingi za kimaadili ni mambo msingi katika mfungamano wa kijamii. Maaskofu wanataka wakuu wa nchi Kaskazini mwa Afrika kuhakikisha kwamba, wanaendeleza na kudumisha misingi hii kama kipimo cha ubora wa mchakato wa demokrasia ya kweli.

Sera na mikakati ya kudhibiti wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, hazina budi kuhakikisha kwamba, zinalinda na kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi. Wananchi wote wahudumiwe pasi na ubaguzi wa kidini, kwani kwa siku za hivi karibuni kuomenekana dalili za Wakristo kutengwa katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, jambo ambalo si haki kabisa. Ikumbukwe kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kumbe, wanapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa na jamii na kwamba, uhuru wa kidini hauna budi kuheshimiwa ili kutoa nafasi kwa Wakristo pia kushiriki katika ibada mbali mbali, lengo ni kushiriki katika mchakato unaopania kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Maaskofu Kaskazini mwa Afrika wanabainisha kwamba, majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ni kati ya vipaumbele vyao vya mikakati na shughuli za kichungaji. Kanisa linapenda kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana katika umoja, upendo na udugu kwa kutambua kwamba, tofauti zao za kiimani ni utajiri mkubwa unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Haya ni majadiliano yanayojikita katika maisha ya watu. Wananchi wawe huru kufuata dhamiri zao nyofu, kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, bila kupoteza utambulisho wao wa kidini.

Maaskofu wanaendelea kubainisha kwamba, wanapenda kujikita katika majadiliano ya kiekumene, ili Wakristo wakiwa wameshikamana na kushibana, waweze kutolea ushuhuda kwa tunu msingi za maisha ya Kikristo katika sala inayomwilishwa kwenye misingi ya haki, amani na upatanisho. Jumuiya za Kikristo Kaskazini mwa Afrika hazina budi kuwa ni maabara ya kiekumene; mahali pa kuwafunda vijana tunu msingi za maisha ya Kiinjili; imani, maadili na utu wema; ili kuweza kumshuhudia Kristo na Kanisa lake kati ya mataifa. Kanisa litaendelea kutoa majiundo ya awali na endelevu ili kuwasaidia vijana kusoma alama za nyakati, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Maaskofu wanapembua kwa kina na mapana shughuli mbali mbali zinazofanywa na Kanisa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa kimsingi wanaionesha ile sura ya Kristo. Kanisa pia halina budi kupewa haki zake msingi na kwamba ni sehemu ya Familia ya Mungu, Kaskazini mwa Afrika na wala si kilaka kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani. Kanisa linapenda kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya watu Kaskazini mwa Afrika.

Maaskofu wanasema kwamba, ndoa mseto ni kati ya changamoto nyingine kubwa inayowakabili katika utekelezaji wa shughuli zao za kichungaji. Licha ya tofauti za kiimani na kitamaduni, ikiwa kama wanandoa wataheshimiana na kuthaminiana, ndoa yao inaweza kuwa ni baraka kubwa ndani ya jamii. Kumbe kuna haja ya kudumisha uhuru wa dhamiri, majadiliano ya kidini, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu. Sera hizi zijioneshe pia katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu. Kanisa linapenda kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili.

Mwishoni, Maaskofu wanawaalika waamini kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, Mama aliyeyakita maisha yake katika sala na kwamba, kilele cha maisha ya kiroho kijioneshe kwa waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wajitahidi kujenga mahusiano mema na jirani zao kama njia ya ushuhuda wa maisha ya imani yanayomwilishwa katika matendo. Waoneshe upendo na ukarimu kwa majirani na maskini kwani Kanisa linapenda kuwakutanisha watu katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili kuwajengea na kuwaimarisha katika imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.