Wosia wangu kwenu: Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu
Jumuiya ya wanafunzi Wakatoliki pamoja na watanzania wanaoishi na kufanya shughuli
zao mjini Roma, tarehe 26 Februari 2015 waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa
na Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, ili kumshukuru Mungu
kwa matendo yake makuu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo Katoliki la Shinyanga
kwa kumpata Mchungaji mkuu. Ibada hii imefanyika kwenye Kikanisa cha Chuo cha Mtakatifu
Paulo, mjini Roma.
Katika mahubiri
yake, Askofu mteule Sangu, amewataka Mapadre na Watawa kwa namna ya pekee kabisa kujenga
na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwani hapa ni mwanzo na kilele cha
maisha na utume wa Kanisa. Anatambua kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inawasaidia
kupyaisha maisha, utume na dhamana ambayo wamekabidhiwa na Mama Kanisa katika maisha
yao.
Muda wa saa moja, unatosha kabisa kukaa mbele ya Ekaristi Takatifu ili
kuzungumza na Kristo pamoja na kumwachia nafasi ya kukushirikisha mapenzi yake katika
maisha na utume wako. Kwa njia ya Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, watafanikiwa
kuwagusa na kuwasaidia watu katika hija ya maisha yao ya kiroho na kimwili. Mapadre
na Watawa wajifunze kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na watakatifu wengine
wa Kanisa waliotumia muda wao mwingi kuabudu Ekaristi Takatifu.
Huu ndio wosia
na zawadi kubwa ambayo Askofu mteule Libertaus Sangu amependa kuiachia Jumuiya ya
Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, wakati huu anapoanza ukurasa mpya wa maisha
yake kama Mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Askofu mteule Sangu
anasema kwamba, Mwenyezi Mungu daima anasikiliza sala za waja wake na kuzijibu kwa
wakati muafaka. Kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki
Shinyanga ni matokeo ya sala na sadaka ya Familia ya Mungu Jimboni Shinyanga, iliyosali
na kumlilia Mwenyezi Mungu ili awapatie Mchungaji mkuu baada ya kufariki kwa Askofu
Aloysius Balina, zaidi ya miaka miwili iliyopita. Mwenyezi Mungu anasikiliza sauti
ya waja wake hata katika udhaifu wao na atawajibu kwa wakati wake.
Askofu mteule
Sangu anasema kwamba, waamini hawana budi kumwilisha sala katika maisha na vipaumbele
vyao sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, jambo ambalo wakati
mwingine si rahisi sana. Anasema, amekubali kuwa Askofu wa Shinyanga kama sehemu ya
utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha
yake na kwamba, anajiaminisha mikononi mwake Yeye aliyemteua kwa matumaini kwamba,
atamwezesha kutekeleza wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakasa Watu wa Mungu
kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.