2015-02-28 10:42:52

Vikwazo vya maendeleo endelevu!


Jumuiya ya Kimataifa imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika haki ya maendeleo, wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbu kumbu ya miaka thelathini, tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Azimio la Haki ya Maendeleo.

Lakini ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Kimataifa hadi leo hii inakabiliwa na changamoto kubwa za maendeleo kutokana na umaskini mkubwa wa hali na kipato, unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu wapatao billioni 2.2, sawa na asilimia 15% ya idadi ya watu duniani.

Bado kuna umati mkubwa wa watu ambao hawana huduma bora za afya, elimu na kwamba, wanaishi katika mazingira magumu, kiasi kwamba, kuna pengo kubwa kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Kuna vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutishia usalama wa maisha na mali za watu bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na myumbo wa uchumi kimataifa. Kimsingi, haya ni mambo yanayochangia kukwamisha mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu duniani.

Haki ya maendeleo kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa haina budi kujikita katika umoja, mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa kutambua kwamba, wote wanaunda familia ya binadamu; usawa, utu na heshima ya binadamu; matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya mafao ya wengi; maendeleo yanapaswa kumshirikisha mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, binadamu anapaswa kuwa ni dira ya mipango na mikakati ya maendeleo kiuchumi na kijamii. Ili kuwa na uwiano mzuri wa maendeleo, kuna haja ya kujikita katika kanuni ya auni na mshikamano.

Mambo haya yanategemeana ili kusongesha mbele mchakato unaopania kumletea mwanadamu maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Huu ni mchango wa kina uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao yake makuu mjini Geneva, katika mkutano wa kumbu kumbu ya miaka thelathini tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Azimio la Haki ya Maendeleo. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi sana katika mchakato wa maendeleo endelevu kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko.

Ukosefu wa usawa kati ya watu ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha chuki na kinzani nyingi za kisiasa na kijamii. Utu na heshima ya binadamu viwe ni dira katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo kiuchumi na kisiasa duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa wadau mbali mbali, vinginevyo, uchoyo na ubinafsi vitatawala na hivyo kusababisha majanga katika maisha ya watu. Mshikamano ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mchakato wa maendeleo na mafao ya wengi. Hiki ni kielelezo makini kinachotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya binadamu na wala si vitu, ili kuondokana na tabia ya uchu wa mali inayopata chimbuko lake katika ubinafsi na uchoyo.

Ikumbukwe kwamba, kila binadamu ana haki na wajibu wa kujipatia maendeleo, kwani hii ni sehemu ya haki yake kama inavyobainishwa na Umoja wa Mataifa; kwa kuheshimu usawa, huku mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati yote hii, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapokabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira na uwepo wa wimbi kubwa la wahamiaji linalotafuta nafuu na ubora wa maisha.

Mikakati ya maboresho katika biashara ya kimataifa inaweza kusaidia kupunguza baa la umaskini duniani pamoja na kuendeleza mchakato wa maboresho ya hali ya maisha ya watu katika Jamii. Kumbe, mikakati ya maendeleo kwa siku za usoni haina budi kuvalia njuga mambo ambayo yanaendelea kusababisha baa la umaskini, njaa na maradhi duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira; kwa kuboresha nguvu kazi ili kuzalisha kwa tija, ubora na viwango; kwa kulinda na kuendeleza familia kama kikolezo muhimu katika mchakato wa maendeleo ya binadamu: kiuchumi na kijamii.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, haina budi kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano na kuondokana na na mwelekeo wa sasa wa sera na mikakati ya kiuchumi isiyojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahii ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.