2015-02-28 15:34:38

Ujenzi wa nyumba bora!


Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza ujenzi wa nyumba 14 za kisasa kwa ajili ya watumishi wa Halmashauri ya Busokelo ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa nyumba za watumishi kwenye halmashauri hiyo mpya. Nyumba hizo 14 ni sehemu tu ya mradi mzima wa kujenga nyumba 50 katika Kata ya Lwangwa ambazo pia zitauzwa kwa wananchi. Mradi huo unakadiriwa kutumia sh. bilioni 1.1 ikiwa ni wastani wa sh. milioni 79 kwa kila nyumba.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Ijumaa, Februari 27, 2015 kwenye uwanja wa shule ya msingi Lwangwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imeridhia kuanza kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa kwenye Halmashauri hiyo ili kuisaidia iondokane na tatizo la ukosefu wa nyumba bora. “Kuanza kwa mradi huo kutawezesha watumishi na wakazi wa Busokelo, kupata fursa ya kukopa au kununua nyumba hizo zipatazo 50, zitakazojengwa na Shirika la letu la Nyumba,”alisema.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu iliridhia maombi ya halmashauri hiyo kukopa fedha ili kugharamia mradi huo baada ya kujiridhisha kuwepo kwa mahitaji makubwa ya nyumba za kisasa kutokana na ukuaji wa kasi wa mji huo. “Busokelo ni miongoni mwa halmashauri zilizoanzishwa kwa kipindi cha muda mfupi kutokana na kasi yake ya ukuaji na ustawi wa wananchi hivyo, ni jukumu la Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya kuufanya mji huu uonekane wa kisasa zaidi,”alisema.

Mradi huo ulioanza Julai 2014, unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu, ambapo halmashauri hiyo tayari imekwishalipa sh. milioni 500 kugharamia shughuli za ujenzi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Prof. Mark Mwandosya ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki, alisema halmashauri itaweza kujiongezea kipato kupitia mradi huo kwa kuutumia kama sehemu ya chanzo cha kodi. Prof. Mwandosya aliwataka wakazi wa jimbo hilo kuchangamkia fursa hiyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.