2015-02-28 10:39:12

Mshikamano katika mchakato wa Uinjilishaji!


Kuanzia mwaka 1959, Kanisa linaadhimisha Siku ya Wahispania wanaofanya utume wao Amerika ya Kusini, sherehe ambayo kwa mwaka 2015 inaadhimishwa tarehe Mosi Machi, yaani Jumapili ya kwanza ya Mwezi Machi. Wainjilishaji kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ndiyo kauli mbiu inayotolewa na Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini. RealAudioMP3

Hii ni siku ambayo Kanisa Katoliki nchini Hispania linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa kuchangia kwa hali na mali shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Wamissionari kutoka Hispania huko Amerika ya Kusini.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya Wamissionari wapatao 9,000 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi za Amerika ya Kusini, kwa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Kardinali Ouellet anasema kwamba, Siku ile ya Pentekoste, Mitume waliokuwa wamejifungia kwa hofu ya Wayahudi, walipata nguvu na ari mpya iliyowasukuma kutoka nje ili kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa moyo mkuu bila woga wala makunyanzi, wakathubutu kuwa ni Wamissionari wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu.

Mchakato huu hauna budi kuendelezwa na Wamissionari wanaoendelea kujisadaka katika nchi za Amerika ya Kusini kwa kujikita katika Injili ya Furaha na Ujasiri kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika nyaraka zake mbali mbali. Furaha ni chemchemi inayobubujika kutoka kwa Wainjilishaji, ambao kimsingi wanapaswa kuwashirikisha wale wanaowainjilisha. Kumbe, Uinjilishaji wa watu hauna budi kujikita katika furaha, ukarimu na upendo wa dhati, huku Wainjilishaji wenyewe wakionesha ushupavu wa kutangaza Injili pasi na kukata tamaa wala kuchoka.

Kardinali Ouellet anasema kwamba, hakuna hata kidogo nguvu ya kimissionari iliyotolewa kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu kwa upendo na mshikamano itakayoweza kupotea bure. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, matunda ya Uinjilishaji hayategemei nguvu na juhudi za kibinadamu. Ni Yesu Kristo anayewapatia nguvu ya kuendeleza mikakati na shughuli za Uinjilishaji, hadi kuwafikia watu wanaoishi pembezoni mwa maisha, ili wao pia waweze kuona mwanga wa Injili.

Kanisa linatambua magumu na changamoto ambazo Wamissionari wanakumbana nazo katika maisha na utume wao; kuna mazingira ambayo yamekuwa ni kizingiti kikuu cha Uinjilishaji, lakini Wamissionari watambue kwamba, nguvu, juhudi na maarifa waliyowekeza katika mchakato wa kuwatangazia Watu Injili ya Furaha hazitaweza kupotea kamwe, kama ilivyo vigumu kupoteza upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Ouellet anawaalika Wamissionari kufanya hija pamoja na Yesu Kristo kila siku ya maisha yao, huku wakimwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwapatia dira na mwongozo katika utekelezaji wa dhamana hii nyeti. Waendelee kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu kwa kutambua kwamba, Yesu daima yuko pamoja nao kamwe hatawaacha yatima.

Ni jukumu la Wamissionari kuwatangazia watu Injili ya Kristo hata ikibidi kwenda kinyume cha maelekeo ya kijamii, kwani wao kimsingi ni sauti ya kinabii. Wamissionari wasikubali kupokwa furaha ya Uinjilishaji kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Wamissionari waanze na kuhitimisha siku ya maisha na utume wao kwa kukutana na kuzungumza na Yesu Kristo katika Neno na Sakramenti, ili kuimarisha imani na furaha ya kukutana na Yesu huko Amerika ya Kusini.

Wamissionari kamwe wasikubali kukatishwa tamaa kutokana na magumu mbali mbali wanayokabiliana nayo, wawe na ujasiri wa kuanza tena pale wanapodhani kwamba, wameshindwa na kuanguka, huku wakijitahidi kumwiga Bikira Maria aliyekubali kupokea na kuumwilisha mpango wa Mungu katika maisha yake. Wamissionari wathubutu kuendelea kuutafakari uso wa Mungu kwa njia ya huduma makini kwa jirani pamoja na kumwilisha sala katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Kardinali Ouellet anawakumbusha Wamissionari kwamba, wanatumwa na Mama Kanisa kuwaendelea Watu wa Mataifa, kwani utume wa Kanisa ni kielelezo cha upendo wa Kristo kwa waja wake. Utume wa Uinjilishaji ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Watu wa Mungu kwa ajili ya wote pasi ubaguzi wa watu au hali yao ya kijamii. Utambulisho wa kimissionari ujioneshe katika huduma kwa waamini, kwa kuwatakia mema na furaha ya kweli.

Kardinali Marc Ouellet anahitimisha ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wahispania wanaofanya utume wao Amerika ya Kusini kwa kusema kwamba, mlchakato wa Uinjilishaji Amerika ya Kusini ni changamoto ya kuwaendelea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wamissionari wajidhaminishe chini ya usimamizi na tunza ya Bikira Maria, ili kweli juhudi zao za kimissionari ziweze kuwa ni kielelezo cha utii kwa Mungu Baba Mwenyezi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.