Boko Haram na utandawazi vinatishia familia nchini Nigeria
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba, Familia ni shule ya kwanza
ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni; ni Kanisa dogo la nyumbani;
mahali ambapo waamini wanajifunza: utakatifu, upendo na msamaha wa kweli. Lakini familia
nchini Nigeria zinakabiliana na changamoto nyingi na kati ya hizi ni kwamba, familia
nyingi zimemezwa mno na malimwengu na kwamba, mfungamano wa maisha na tunu bora za
kifamilia unavurugwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanyofanywa na Kikundi cha Boko
Haram, ambacho kwa sasa ni tishio la maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, athari za utandawazi na maendeleo ya
sayansi na teknojia zinajionesha kwa namna ya pekee nchini Nigeria. Matumizi ya mitandao
ya kijamii ambayo kimsingi ilipaswa kuwaunganisha watu kwa sasa inaonekana kuwa ni
kati ya "majanga" ya kifamilia, kwani matumizi mabaya ya mitandao yamepelekea uaminifu
na udumifu katika maisha ya ndoa na familia kulega lega, kiasi kwamba, ndoa nyingi
zinaendelea kuvunjika. Maaskofu wanawahimiza wanafamilia kuwa na matumizi bora na
sahihi ya mitandao ya kijamii.
Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko
Haram yanaendelea kupandikiza mbegu ya: kifo, chuki na uhasama kati ya wananchi wa
Nigeria. Mashambulizi haya pamoja na homa ya uchaguzi mkuu nchini humo ni kati ya
mambo ambayo kwa sasa yanazikosesha familia nyingi amani na utulivu wa ndani. Watu
wengi wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi
haya kiasi cha kuwakatisha watu tamaa! Kuna wanawake na wasichana wanatekwa na kunyanyaswa
kijinsia; mambo yote haya yanadhalilisha utu na heshima ya wananchi wa Nigeria. Kutokana
na kuhofia usalama wa maisha, kuna kundi kubwa la watoto ambalo limepotezana na wazazi
pamoja na walezi wao.
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linalaani sana vitendo
vya Kikundi cha Boko Haram kuwatumia watoto kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kuwafungia
mabomu ya kujilipua. Huu ni unyama wa hali ya juu kabisa ambao kamwe hauwezi kuvumiliwa.
Baadhi ya wanasiasa uchwara na waliofilisika kwa kumezwa mno na uchu wa mali na madaraka,
wamekuwa wakiwatumia vijana nchini Nigeria kufanya vurugu na kuvunja amani; mambo
ambayo yanabomoa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kuwafanya vijana
wengi kukosa dira na mwelekeo wa maisha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria
linaiomba Serikali pamoja na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa uhuru na
usalama kwa familia ili ziweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa kuwapatia watoto
malezi na elimu bora itakayowasaidia kupambana na maisha kwa sasa na kwa siku za usoni.
Vita na kinzani za kijamii ni mambo ambayo hayana budi kudhibitiwa, ili haki, amani
na maridhiano yaweze kutawala tena nchini Nigeria.