Pato Ghafi la Taifa (GDP) nchini Tanzania katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka
2014 limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 21.2 kutoka shilingi trilioni 19.8
za kipindi kama hicho kwa mwaka 2013. Akizungumza na waandishi wa habari jiji Dar
es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw.
Morrice Oyuke, amesema kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2014 sekta nyingi
za uchumi zimefanya vizuri katika uzalishaji ikilinganishwa na mwaka 2013.
Amesema
katika kipindi hicho shughuli za uchimbaji wa Madini , Mawe na Kokoto zimekua kwa
asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 3.3 za mwaka 2013, Uzalishaji wa bidhaa za
viwandani ukikua kwa asilimia 10.8 kutoka asilimia 10.4 pamoja na ongezeko la uzalishaji
wa umeme kwa asilimia 10.7 kutoka asilimia 10.3 za mwaka 2013 kutokana na matumizi
ya mafuta na Gesi.
Amezitaja sekta nyingine kuwa ni usambazaji maji ambao umekua
kwa asilimia 12.7 kutoka 6.9 za mwaka 2013, Habari na Mawasiliano kwa asilimia 11.9
kutoka 7.0, Shughuli za Fedha na Bima zikikua hadi kufikia asilimia 13.9 kutoka asilimia
6.8 za mwaka 2013. Ameongeza kuwa katika kipindi hicho huduma za upangishaji wa nyumba
zilikua hadi kufikia asilimia 2.2 kutoka 2.1, shughuli za kitaalamu, kisayansi, ufundi
na utawala zikifikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 1.0 ya mwaka 2013.
Bw. Oyuke
amezitaja shughuli nyingine kuwa ni uendeshaji wa Serikali ambazo zilikua kwa asilimia
4.9 ikilinganishwa na 4.4, huduma za Elimu kwa asilimia 3.7 kutoka 3.5, Afya kwa asilimia
8.1 pamoja na shughuli za Sanaa na Michezo ambazo zilikua kwa asilimia 2.5 ikilinganishwa
na 1.6 ya mwaka 2013. Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa Almasi katika kipindi
cha robo tatu ya mwaka 2014 ulikuwa karatasi 66,508 ikilinganishwa na karatsi 27,828
zilizozalishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2013.
Akizungumza kuhusu sekta
ambazo hazikufanya vizuri katika kipindi cha Robo tatu ya mwaka 2014 Mkurugenzi huyo
amesema kuwa ni dhahabu ambayo uzalishaji wake ulifikia Kilogramu 10,137 kwa mwaka
2014 ikilinganishwa na 11,010 za mwaka 2013,Madini ya Tanzanite kilogramu 1,449 kutoka
5140 zilizozalishwa mwaka 2013.
Amefafanua kuwa shughuli za Biashara za Jumla
na reja reja, Ukarabati wa magari na pikipiki pamoja na vifaa vingine vya nyumbani
zimeonyesha kukua kwa asilimia 6.0 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na kasi ya asilimia
6.7 ya mwaka 2013, shughuli za uhifadhi asilimia 13.9 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa
na asilimia 19.3 za mwaka 2013.
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi hicho
cha miezi mitatu ya mwaka 2014 kuanzia Julai mpaka Septemba, Pato la taifa kwa bei
za mwaka 2007 limefikia kiasi cha Shilingi trilioni 10. 7 ikilinganishwa na shilingi
trilioni 10.1 ya mwaka 2013.