2015-02-27 09:10:00

Msiogope kushikamana na kuwatetea maskini!


Maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu kwa kusoma alama za nyakati ili kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya kuwashangaza viongozi wa Kanisa katika maisha na utume wao kama ilivyotokea kwa Nabii Eliya alivyomshangaza yule Mjane wa Sarepta kwa kumponya mwanaye aliyekuwa amemsababishia uchungu mkubwa moyoni mwake. Mama Mjane anatambua na kukiri ukuu wa Mungu katika maisha yake.

Hii ndiyo changamoto ambayo imetolewa na Padre Bruno Secondin wakati wa tafakari zake kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu wakati wa mafungo ya maisha ya kiroho huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Vatican, mafungo ambayo yalianza Jumapili jioni na kuhitimishwa, Ijumaa asubuhi tarehe 27 Februari 2015, kwa Ibada ya Misa Takatifu. Hapa Kanisa linawaangalia maskini jinsi wanavyoshiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kujikita katika imani, matumaini na mapendo.

Ni kundi linaloonesha ukarimu hata katika umaskini wake, kiasi cha kumshangaza Nabii Eliya ambaye alionekana kuwa na shingo ngumu. Mjane wa Sarepta kwa namna ya pekee, anawafundisha waamini kwamba, umaskini na fumbo la kifo ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa kikamilifu bila ya kupoteza utu na heshima ya binadamu! Mjane wa Sarepta hatua kwa hatua anakutana na uso wa Mungu mwenye huruma na mapendo anayekuja kuganga na kuponya madonda ya machungu katika maisha yake. Hapa haki ya Mungu inajionesha na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kielelezo makini kwa wafuasi wa Kristo, kwani maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wana upendeleo wa pekee mbele ya Yesu na Kanisa lake.

Padre Secondin anasema, Nabii Eliya alikuwa ni mtu wa haki na kamwe hakusita kusema na kusimamia ukweli kiasi hata cha kumkaripia Mfalme Ahazi kwa kumnyang'anya na kumdhulumu Nabothi shamba ambalo lilikuwa ni urithi kutoka kwa Baba zake. Lakini ni mara ngapi kilio cha maskini kimeweza kusikiwa na wakuu wa watu? Kilio cha damu kinaendelea kusikika huko Mashariki ya Kati, Afrika na sehemu mbali mbali za dunia, lakini watu wamekaa kimya kana kwamba, hakuna kinachotendeka, hiki ni "kilio cha samaki machozi yamebaki majini"

Padre Secondin anasema, viongozi wa Kanisa kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema, hawana budi kuungana ili kulinda, kutetea na kusimamia haki msingi za maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, ardhi ni mali ya Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Toba na wongofu wa ndani vipate mwanzo wake katika maisha ya viongozi na waamini kwa ujumla kwa kubadili mfumo wa maisha kwa kuanza kujikita katika ukweli na uwazi; haki na uaminifu kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma na wala si ndoana ya kujitafutia "ujiko".

Viongozi wa Kanisa watekeleze dhamana na wajibu wao barabara; kwa kuhamasisha kulinda na kutunza mazingira; kwa kuwatetea na kuwahifadhi wakulima wadogo wadogo wanaopokonywa ardhi na vyanzo vya maji kwa ajili ya mafao ya wajanja wachache katika jamii. Viongozi wawe na ari pamoja na ujasiri wa kupinga nyanyaso, dhuluma na uonevu ndani ya jamii; kwa kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kujikita katika kanuni msingi za Kiinjili bila woga wala makunyanzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.