Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kufufua bandari ndogo
14 kwenye mikoa mitatu inayozunguka Ziwa Nyasa ili kuimarisha usafiri wa majini
kwa wakazi wa Ruvuma, Njombe na Mbeya. “Tangu mwaka 2006 bandari za kwenye mikoa ya
Ruvuma, Njombe na Mbeya zilikufa na hivyo kuleta shida ya usafiri kwa wakazi wa maeneo
hayo lakini Serikali imeamua kuzifufua bandari hizo na Itungi itakuwa ndiyo kituo
kikuu cha bandari zote katika Ziwa Nyasa,” alisema Waziri Mkuu.
Alikuwa
akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kyela kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jumatano,
Februari 26, 2015 kwenye uwanja wa michezo wa Mwakangale na kuhudhuriwa na maelfu
ya wakazi wa wilaya hiyo. Alizitaja bandari hizo kuwa ni Ndumbi, Lundu, Njambe, Mkili,
Liuli, na Mbamba bay ambazo ziko mkoani Ruvuma. Nyingine ni Lumbila, Ifungu, Nsisi,
Lupingu na Manda ambazo ziko Njombe wakati bandari za Mbeya ni Itungi, Kiwira na Matema.
Alisema
ili kufanikisha hilo, Serikali imehamisha chelezo (Dry Dock) kutoka bandari ya Mwanza
na kwamba mkandarasi kutoka Kampuni yaSongoro Marines, ameshaanza ujenzi wa chelezo
hiyo. “Baada ya kukamilika, Chelezo hiyo, itatumika kutengenezea meli mpya yenye uwezo
wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo na kufanya ukarabati wa meli pindi zinapohitaji
matengenezo. Nimeambiwa na mkandarasi kutaka watamaliza hii kazi ifikapo Juni, mwaka
huu,” alisema huku akishangiliwa na umati huo.
Waziri Mkuu alisema, mbali
ya hilo, chelezo hiyo pia itatumikakutengeneza matishari mawili ya kubebea mizigo
ambayo yatakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 1,000 kila moja. “Yatatumika kusafirisha
mizigo hiyo hususan mazao ya wakulima kupitia bandari ndogo zilizopo lakini pia yatasafirisha
tani 60,000 za makaa ya mawe, tani 72,000 za saruji kutoka Mbeya kwenda Malawi na
mikoa jirani; tani 10,000 za mbolea kutoka Dar es Salaam pamoja na chuma kutoka Liganga
na Mchuchuma,” alisema.
“Chelezo hiki kitakapokamilika kitakuwa kikubwa
na cha aina yake… hakuna kingine cha kulinganishwa nacho katika nchi jirani za Malawi,
Zambia na Msumbiji. Itumieni fursa hii kwa kutunza ule mto kwenye mdomo wa kuingilia
bandari ya Itungi, msilime kwenye kingo za mto,” aliongeza.
Mapema, akizungumza
na wakazi wa kata ya Lusungo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja
la Lusungo, Waziri Mkuu Pinda alisema daraja hilo ni kiungo muhimu kwenye barabara
hiyo iendayo kwenye bandari ya Matema. Aliwataka wakazi wa kata hiyo walitunze daraja
hilo ili liweze kuwasaidia kusafirisha bidhaa na mazao wanayolima. Ujenzi wa daraja
hilo, ambalo limejengwa kupitia mfuko wa barabara, lina urefu wa mita 50 na upana
wa mita 7.3 pamoja barabara yenye urefu wa mita 600 kutoka kwenye maingilio ya daraja
hilo, limegharimu kiasi cha sh. bilioni 3.7 huku ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa
asilimia 99%.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda alipewa jina la
MWAKABULUFU na Chifu Ernest Mwailemale wakati akisimikwa kuwa kiongozi wa eneo hilo
la Lusungo. Waziri Mkuu alivishwa mgolole na kupewa mkuki ili autumie kuilinda nchi
dhidi ya maadui kutoka pande zote. Akizungumza mara baada ya kumsimika Waziri Mkuu,
Chifu Mwailemale mwenye umri wa miaka 91, alisema jina hilo ni la babu yake mzaa baba
ambaye aliwahi kutawala eneo hilo. Hata hivyo, hakutaja ni mwaka gani.
Alipoulizwa
maana ya jina hilo, Chifu Mwailemale ambaye wakati wote alikuwa akizungumza Kiswahili
kwa ufasaha alisema: “Jina hili halina maana maalum bali na heshima kwa sababu lilikuwa
la Chifu aliyetawala eneo hili,” alisema na kufafanua kuhusu umri wake: “Nina miaka
91 kwa maana nilizaliwa tarehe 25 Septemba mwaka 1924,” alisema Chifu huyo ambaye
anaelezwa kupigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
MIMBA, UTORO KYELA VYAMTISHA
WAZIRI MKUU
* 94 wapewa ujauzito, 645 watoroka shule wilayani humo
Waziri Mkuu Mizengo
Pinda amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
hiyo kuwasaka na kuwakamata wale wote waliowapa ujauzito wanafunzi na kuwafikisha
mahakamani mara moja ili liwe fundisho kwa wengine. Akizungumza kwa nyakati tofauti
kwenye shule ya sekondari ya Mwaya, kwenye kata za Ikusya na Lusungo na wakazi wa
mji wa Kyela, Jumatano, Februari 26, 2015), Waziri Mkuu alisema elimu ni jambo la
msingi sana kwa kizazi cha sasa na kijacho na Serikali haiwezi kuona fursa za elimu
zikichezewa kiasi hicho. “Haiwezekani hata kidogo! Serikali hatuwezi kuwa tunahimiza
ujenzi wa madarasa kila kukicha halafu watoto wanaopaswa kusoma kwenye hizo shule
wao wanatoroka. Hawa watoto wana wazazi, iweje kuwe na utoro kiasi hiki?” alihoji.
“DED
na DC wabaneni wazazi na mabinti walioharibiwa masomo, ni lazima watawataja wanaume
waliohusika kuwapa mimba. Kwa kuanzia anzeni na hao wa mwaka jana ambao ni wasichana
11. Wakiwekwa ndani wachahe itakuwa fundisho kwa wengine,” alisema. Akielezea ukubwa
wa wa tatizo hilo kwenye shule za sekondari peke yake, Waziri Mkuu alisema mwaka 2010,
wasichana 26 walipewa ujauzito; mwaka 2011 (wasichana 22); mwaka 2012 (wasichana 19);
mwaka 2013 (wasichana 16) na mwaka 2014 (wasichana 11). “Jumla yao ni 94, hii ni idadi
kubwa sana. Akina baba waacheni watoto hawa wamalize masomo, msiwaharibie maisha,”
alikemea.
Akichanganua takwimu za utoro kwa wanafunzi haohao wa sekondari,
Waziri Mkuu alisema mwaka 2010 walitoroka wanafunzi 95; mwaka 2011 (wanafunzi 160);
mwaka 2012 (wanafunzi 212); mwaka 2013 (wanafunzi 90) na mwaka 2014 (wanafunzi 88).
“Katika kipindi cha miaka mitano, jumla yao wote hawa ni 645. Hali hii haivumiliki
na jambo liko ndani ya uwezo wa Halmashauri yenu. Fuatilieni wazazi wa hawa watoto
na DC na DED ni lazima tabia hii ikomeshwe mara moja,” alionya.
Aliwaasa
watoto wa wilaya wawe makini na masomo na waache tabia ya utoro na kupenda mambo ya
maisha. “Wanangu someni kwa bidii, achaneni na haya mambo mengine. Ukipoteza nafasi
masomo kidato cha tatu au cha nne, maisha yako yanakuwa yameharibika,” aliwaasa. Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwageukia wanaume wanaowafuata watoto wa shule na kuwataka kimapenzi
wakati wanawake wa wilaya ni wengi kuliko wanaume. “Wlaya hii ina wanaume 106,012
na wanawake 115,478. Sasa ni kwa nini msiwafuate hao akinamama wakubwa ambao ni wengi
kuliko ninyi? Acheni huo mchezo, waacheni hawa watoto wa kike wamalize masomo yao,”
alisisitiza.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya
Kyela, Bi. Margareth Malenga alisema kushamiri kwa biashara kwenye mpaka wa Kasumulu,
mkoani Mbeya, kumechochea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaotoroka shuleni na
kwenda kujishughulisha na biashara ndogondogo mpakani hapo.
“Aidha, kukosekana
kwa chakula kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani hamu, ni sababu
nyingine inayofanya wanafunzi waache masomo na kwenda kufanya biashara ndogondogo
kwenye mpaka wa Kasumulu,” aliongeza. Alisema hali hiyo imechangiwa na kuwepo kwa
baadhi ya kaya masikini zinazoshindwa kuwalipia gharama za masomo watoto wao. Akifafanua,
Bi. Malenga alisema katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, wavulana 414 na wasichana
159 waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari waliacha shule kwa sababu za utoro.
Kuhusu
elimu ya msingi, Bi. Malenga alisema, wanafunzi wapatao 711 wametoroka shule lakini
kutokana na jitihada zilizofanyika, wanafunzi 155 wamerudishwa shuleni. “Wanafunzi
556 waliobakia wanaendelea kutafutwa kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili waweze
kuwarudishwa kuendelea na masomo,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema wameanzisha
utaratibu wa kila Mkuu wa Shule kuwasilisha ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi kwa
watendaji wa kata na vijiji kila Ijumaa ambapo tangu utaratibu huo uanze, wamefanikiwa
kudhibiti utoro kwa asilimia 91%.