2015-02-27 09:09:43

Kuhusu biashara haramu ya binadamu? Kanisa lina neno!


Kardinali John Atcherley Dew, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Wellington, New Zealand anasema, nchini mwake, Kanisa linakabiliana na changamoto kubwa za athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia usalama, ustawi na maendeleo ya wananchi wa New Zealand; wimbi kubwa la wahamiaji wanaotafuta fursa bora za maisha pamoja na ukarimu kwa watu kutoka katika mataifa na tamaduni mbali mbali wanaotafuta fursa za ajira na makazi nchini New Zealand.

Kardinali Dew anasema, kuteuliwa kwake kama Kardinali na hatimaye kusimikwa na Baba Mtakatifu ni kielelezo cha kutambua mchango na dhamana inayotolewa na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa New Zealand, kiroho na kimwili. Eneo hili la dunia linakabiliwa na changamoto ya biashara haramu ya binadamu na kwamba, Kanisa hapa haliba budi kujifunga kibwebwe ili kupambana na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia, New Zealand ilipata wimbi kubwa la wahamiaji na wageni kutoka Barani Ulaya, lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, wahamiaji wengi ni wale wanaotoka Barani Asia, changamoto kwa waamini walei kuhakikisha kwamba, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wanaweza kusaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya. Wasaidie kupambana na changamoto za maisha kwa kujikita katika Mafundisho ya Kanisa, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Ili kutekeleza dhamana hii, Wakristo hawana budi kupewa majiundo makini ya awali na endelevu, ili kuwawezesha kuwa imara na thabiti katika maisha na utume wao duniani; tayari kuwashirikisha jirani zao Injili ya Furaha, Amani na Matumaini. Kanisa linaendelea kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, ukarimu na mapendo kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na kujitahidi kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinajionesha kwa kuongezeka kina cha bahari, hali inayotishia usalama wa maisha na maendeleo ya watu, changamoto ya kulinda na kutunza mazingira. Kanisa linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendelea kutekeleza wajibu wao barabara, kwani binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji.

Kardinali Dew anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni fursa ya kuendeleza miito mitakatifu. Kuna umati mkubwa wa vijana wanaotaka kujiunga na maisha ya kitawa nchini New Zealand. Kila mwamini anapaswa kufanya tafakari ya kina kuhusu wito wa maisha yake pamoja na kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuona umati mkubwa wa Watawa ukijisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani; ushuhuda wa utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini New Zealand.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.