2015-02-27 15:30:31

Injili ya Kristo ni chemchemi ya furaha!


Furaha ya Injili inaujaza moyo na maisha ya mwamini ndiyo kauli mbiu ambayo inaongoza mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa mjini Vatican kwa viongozi wa Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa tafakari ya kina zaidi katika Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium, dira na mwongozi wa maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huu.

Padre Cantalamessa katika mahubiri yake, Ijumaa, tarehe 27 Februari 2015 amegusia kuhusu umuhimu wa waamini kukutana na Yesu wa Nazareti; changamoto zinazowakabili Wakristo katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa; Injili kama chemchemi ya furaha kwa moyo na maisha ya mwamini inayowawajibisha kutambua imani, matendo na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kitume, Injili ya Furaha anasema kwamba, Mkristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo anapewa wajibu wa Kimissionari, kumbe anapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kuanzia ndani ya familia, kama shule ya kwanza ya Unjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mwamini katika medani mbali mbali za maisha hana budi kujibidisha kukutana na Yesu Kristo katika maisha yake; kwa kupania na kutekeleza dhamana hii katika uhuru kamili pasi na shuruti ya kisheria au mazoea.

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maisha ya Wakristo tangu kutoka katika Kanisa la mwanzo, Wakristo walipopewa uhuru wa kuabudu na katika maeneo ikawa ni dini rasmi hadi wakati huu ambapo kuna kinzani kubwa kati ya imani na maisha ya kijamii. Hapa ndipo Baba Mtakatifu Francisko anapokita dhamana ya Uinjilishaji mpya unaomwezesha mwamini kufanya maamuzi mazito katika maisha yake ya kiimani kwa njia ya ushuhuda makini; huu ndio Ukristo unaomwilishwa katika matendo!

Historia ya Kanisa inaonesha kwamba, Kanisa limekuwa makini katika kuwafunda watoto wake wanaotaka kupokea Sakramenti ya Ubatizo na baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumeibuka vyama vingi vya kitume, ili kuwasaidia waamini kuuishi Ukristo wao barabara badala ya kuwa ni Wakristo wa majina. Mkazo ukawekwa katika mshikamano ndani ya Kanisa, ili kumwezesha Roho Mtakatifu kuliongoza Kanisa na Wakristo kujazwa furaha ya Injili katika mioyo na maisha yao, changamoto ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kwa Kristo na Kanisa lake.

Hapa toba na wongofu wa ndani ni mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza ili kuweza kupata furaha ya Injili inayoburudisha moyo na kuneemesha maisha ya mwamini katika mwelekeo mpya zaidi, ili kupata maisha ya uzima wa milele. Toba imwezeshe mwamini kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya imani, ili kweli waweze kuwa ni watoto wake wapendwa, kwani mambo yote yaliyokuwa faida kwao sasa wanaweza kuyahesabu kuwa ni hasara kwa ajili ya Kristo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, ili waonekane katika Yeye, kwa kutokuwa na haki yao wenyewe, ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, hali itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani.

Padre Cantalamessa anabainisha kwamba, Injili ni chemchemi ya furaha inayojikita katika neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawezesha waamini kukutana na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, ili waweze kupata utimilifu wa maisha. Imani inamwilishwa katika matendo na imani bila matendo hiyo imekufa! Waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo.

Hapa Baba Mtakatifu anasema, imani na matendo ni chanda na pete inayomwezesha mwamini kupinga ubinafsi, ukosefu wa haki na kukataa katu katu kumezwa na malimwengu kwa kupenda mno madaraka, fedha na mali; bali kuwa tayari daima kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; hapa Uinjilishaji na Utakatifu wa maisha vinakwenda hatua kwa hatua, kiasi hata cha kuweza kuvumilia shida na madhulumu ya kiimani, kwani hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayewaimarisha katika udhaifu wao. Injili ni matunda ya Roho Mtakatifu yanayopaswa kuendelezwa na kudumishwa!

Waamini wanakumbushwa kwamba, Roho Mtakatifu anawasaidia kupyaisha maisha yao kwa njia ya: Sala na tafakari ya Neno la Mungu; kwa maisha ya Kisakramenti, toba na wongofu wa ndani; lakini zaidi katika hali ya ukimya inayowawezesha waamini kumwilisha imani inayobubujika kutoka katika Habari Njema ya Wokovu katika matendo ya huruma. Kwaresima anasema Padre Raniero Cantalamessa ni kipindi cha kumwachia nafasi Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza na hatimaye, kutoa harufu nzuri ya ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.