2015-02-26 10:48:40

Zaidi ya watoto 700, 000 wanaishi katika mazingira hatarishi!


Taarifa kutoka Sudan ya Kusini zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto laki saba wanaoishi katika mazingira hatarishi, wengi wao ni watoto wanaotoka katika maeneo ya vita na kinzani za kijamii kama vile: Darfur, Kordofan ya Kusini na Blue Nile.

Ni watoto ambao wameachwa bila ulinzi wala tunza ya wazazi na walezi wao kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyowalazisha wananchi kukimbilia na kuacha makazi yao kwa kuhofia usalama wao wa maisha. Katika harakati na prukushani hizi, watoto wengi walipoteana na wazazi wao na leo hii wanaishi katika mazingira magumu mjini Khartoum, Sudan Kongwe.

Watoto hawa wanaendelea kunyanyaswa na kutumiwa na watu wasiokuwa wema kwa ajili ya mafao ya binafsi, hatari kubwa kwa siku za usoni. Wadau mbali mbali wanaojisadaka kwa ajili ya kuwalinda na kuwatetea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi wanaiomba Serikali ya Sudan Kongwe kujenga vituo maalum vitakavyotoa msaada kwa watoto hawa, ili kuwajengea tena imani na matumani kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Wizara ya maendeleo na ustawi wa Jamii nchini Sudan Kongwe inasema kwamba, idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi inaendelea kuongezeka maradufu siku hadi siku. Serikali ina mpango wa kufanya maboresho ya maisha kwa ajili ya watoto zaidi ya millioni 10 wanaoishi katika mazingira hatarishi huko Sudan Kongwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.