2015-02-26 10:30:16

Shindeni vishawishi vya uchu wa mali na madaraka!


Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, maafa makubwa ambayo yameendelea kujitokeza nchini humo kuanzia mwaka 2012 ni kutokana na mapungufu ya binadamu, kwa kushindwa kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kusikiliza na kutekeleza mapenzi yake! Hii ni changamoto ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kukumbatia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Askofu mkuu Nzapalainga kwa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Bangui. Vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza kutimua vumbi kunako mwaka 2012 imeacha kurasa chungu na mahangaiko makubwa kwa watu. Wananchi kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa wameanza mchakato wa msamaha na upatanisho wa kitaifa, lakini bado kuna njia ndefu ya kutembea kwa pamoja kama taifa.

Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati inaweza kulinganishwa na Jangwa, mahali ambapo wanahimizwa kupambana kufa na kupona na Shetani pamoja na majaribu mbali mbali, ili amani, upendo na mshikamano wa kitaifa viweze kutawala tena. Ni hija ya maisha ya kiroho inayohitaji kwa namna ya pekee, toba na wongofu wa ndani, kwa nguvu za Roho Mtakatifu wanaweza kushinda tabia ya ubinafsi, uchu wa mali na madaraka.

Ni mwaliko wa kuendelea kujenga na kuimarisha tabia ya majadiliano kati ya watu wa dini, imani na tamaduni mbali mbali, kwa kufanya mabadiliko katika tabia na mtindo wa maisha. Wananchi wajitahidi kujikita katika mchakato wa msamaha na upatanisho, ili amani ya kweli iweze kupatikana. Askofu mkuu Nzapalainga anasema, bado wanaendelea kulifanyia kazi wazo la Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini humo kama kielelezo cha upendo na mshikamano, changamoto na mwaliko wa kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu badala ya kumezwa na chuki na ubinafsi; uchoyo na uchu wa mali na madaraka, mambo yanayosababisha maafa makubwa kwa watu wengi duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.