2015-02-26 10:04:49

Rejeeni kwenye mizizi ya imani, matumaini na mapendo!


Padre Bruno Secondin katika tafakari zake kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Vatican, anaendelea kuwahamasisha kuzingatia mambo msingi katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kujikita zaidi katika ukweli wa ndani, uhuru na hija itakayowawezesha kukumbatia na kusimamia maongozi ya Mungu katika maisha yao.

Ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi unaoweza kumfanya mtu kujikatia tamaa kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya, aliyejichosha, akaingiwa na woga na hatimaye kujikatia tamaa kwa kushindwa kupata mafanikio makubwa aliyokuwa anayatamani moyoni mwake. Viongozi wa Kanisa waondokane na woga usiokuwa na msingi katika maisha na utume wao hali inayoweza kuwasukumiza Katika upweke hasi kiasi cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao. katika hali ya upweke na kujikatia tamaa, waamini wanaweza kujikuta wanajitumbukiza katika ulafi, ulevi, tamaa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Padre Bruno Secondin anawataka viongozi wa Kanisa kuwa na ratiba na mpango mzuri wa maisha na utume wao kwa kuweka uwiano bora kati ya: sala na kazi; mapumziko pamoja na mahusiano ya kijamii. Watambue kwamba, wanahitaji kupumzika, ili kujichotea nguvu kwa ajili ya maisha na utume wao. Katika shida na mahangaiko yao, viongozi wajitahidi kutambua mkono wa Malaika mlinzi unaowaongoza na kuwavusha salama, hapa changamoto ni kurudi katika mizizi ya imani, matumaini na mapendo!

Padre Secondin anawataka waamini kujibidisha kujenga utamaduni wa majadiliano na Mwenyezi Mungu, kwa kujitafua mwanya wa kuchunguza undani wa maisha, ili kuona mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, ni changamoto ya kujifunza kutoka kwa Nabii Eliya kwa kuangalia matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika maisha yao binafsi, maeneo ya kazi na watu mbali mbali. Waangalie mahusiano yao na Mwenyezi Mungu kama ni imara na endelevu au wamekwishamezwa na malimwengu na kutopea katika dhambi?

Waamini wanapaswa kweli kuwa waaminifu kwa maagano waliyofanya mbele ya Mungu, wakiwa na imani na matumaini kwa siku za usoni. Wasiwe kama Nabii Eliya aliyekimbilia Mlimani Oreb, akitaka kukunja jamvi la maisha yake, pale alipoanzia utume wake wa Kinabii, lakini Mwenyezi Mungu akamkirimia nafasi ya kusonga mbele kwa imani na matumaini, kiasi cha kumshangaza Nabii Eliya! Kwake, kifo kingekuwa ni mwisho wa yote!

Ni mwaliko wa kujenga upendo na mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kuwa wakweli na waaminifu kwa karama na zawadi mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha. Kwa namna ya pekee, viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kuanza mchakato wa kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii, ili kugundua mahali ambapo, kweli Mwenyezi Mungu anawangojea!







All the contents on this site are copyrighted ©.