Mshikamano wa umoja na udugu katika mapambano dhidi ya umaskini!
Waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanaweza kushikamana na kusaidiana
katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano,
maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, wote ni wamoja na tofauti zao za
kidini na kiimani ni utajiri mkubwa unaopaswa kutumiwa kwa ajili ya wote pasi na misigano
wala kinzani za kiimani.
Ni katika mantiki hii, Familia ya Mungu nchini Ethiopia
kwa kuzingatia utajiri wa imani za dini na madhehebu mbali mbali yaliyoko nchini humo
wanaendelea kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini na misimamo mikali ya kiimani,
ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni chanzo kikuu cha majanga, sehemu mbali mbali za
dunia. Waamini wa Kanisa Katoliki ni sehemu ya idadi ndogo sana ya Familia ya Mungu
nchini Ethiopia, lakini wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya
wananchi wa Ethiopia hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo jamii yanayozingatia
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kardinali
Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addid Ababa, Ethiopia
katika mahojiano maalum na Gazeti la L'Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican.
Anasema, Wakristo nchini Ethiopia ni daraja la majadiliano ya kidini na kiekumene;
kiasi kwamba, wote wanafanya kazi zao kwa kushirikiana, kuthaminiana na kutegemeana
katika medani mbali mbali za maisha.
Kwa miaka mingi Wakristo na Waislam wanaishi
kwa amani na utulivu pasi na mikwaruzano wala malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko
kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Ethiopia. Kumekuwepo na harakati kutoka
kwa baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kiimani waliotaka kuwagawa na kuwagombanisha
wananchi wa Ethiopia, lakini watu wengi waliowabeza na wala hawakuwafuata katika nia
yao hii mbaya; matokeo yake umoja na mshikamano wa kitaifa unaendelea kudumishwa kama
kikolezo cha maendeleo endelevu.
Kanisa Katoliki nchini Ethiopia ni mdau mkubwa
wa maendeleo katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii anasema Kardinali Souraphiel.
Hapa ni mahali pa kukuza na kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika
uhalisia wa maisha; wakati wa furaha na majonzi. Waamini wamefundwa wakaiva katika
misingi ya imani na wala hakuna tatizo la kutaka kugombea waamini, kwani mfumo huu
wa maisha umepitwa na wakati. Watu wanavuwa na ushuhuda makini wa maisha na wala si
kwa upanga wala mambo mengine yanayopita! Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
inayopokelewa kwa moyo wa unyenyekevu na shukrani.
Kardinali Soiraphiel katika
maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani anasema kwamba, watawa wanaweza kujipambanua
kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika
ustawi na maendeleo ya watu kwa njia ya huduma makini inayotolewa na Mashirika mbali
mbali ya kitawa na kazi za kitume katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.
Kwa njia hii, watawa wanaweza kuwa kweli ni wadau katika kuwatangazia Watu
wa Mataifa Injili ya Maisha, Furaha na Matumaini kwa kukumbatia tunu msingi za maisha,
tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika
kadiri ya mpango wa Mungu. Familia ya Mungu nchini Ethiopia inawaheshimu na kuwathamini
sana watawa kutokana mchango wao katika ustawi na maendeleo ya wengi; ni watu wanaojisadaka
kuwasaidia wazee, watoto yatima na wale ambao wanatumbukizwa katika biashara haramu
ya binadamu na utumwa mamboleo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.