Watawa wanakabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao katika ulimwengu
mamboleo, kiasi kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yanalenga pamoja na
mambo mengine kuwasaidia kuangalia historia iliyopita kwa moyo wa shukrani na kuwa
na matumaini kwa siku za usoni, kwa kuendelea kuwamasisha vijana wa kizazi kipya,
kuona umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao kwa njia ya maisha ya
kitawa!
Hizi ni kati ya changamoto zinazofanyiwa kazi na washiriki wa mkutano
wa kimataifa ulioandaliwa na Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Kitaifa kutoka Chicago,
Marekani, unaofanyika mjini Roma unaofadhiliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton. Padre
David Glenday, Katibu mkuu wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini
Italia anasema, kongamano hili la kimataifa lililofunguliwa Jumatatu, 23 Februari
2015 linawashirikisha wakuu wa mashirika na walezi wa miito kutoka katika mashirika
mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume.
Lengo ni kujaribu kutafuta majibu
muafaka ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya kitawa
bila ya kukata tamaa. Wajumbe wanaendelea kukazia umuhimu wa Kanisa kujikita katika
mchakato wa kuimarisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia ili kupata Familia imara
na thabiti zinazoweza kutoa watoto wenye imani, matumaini na mapendo thabiti, tayari
kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kitawa au Upadre.
Jambo
la kusikitisha ni kuona kwamba, vijana wengi kutokana na changamoto za maisha, wanashindwa
kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuacha yote na kumfuasa Kristo katika
maisha ya kitawa kama ilivyo vigumu hata katika maisha ya ndoa na familia, Changamoto
hizi hazina budi kuangaliwa kwa imani na matumaini pamoja na kuendelea kujielekeza
katika ushuhuda makini, malezi ya awali na endelevu kwa ajili ya udumifu.
Padre
David Glenday anasema, vijana wa kizazi kipya wanahitaji kuona ushuhuda wenye mvuto
na mashiko kutoka kwa watawa; ushuhuda wa furaha na amani ya ndani; ushuhuda unaojionesha
kwa watawa kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii;
ushuhuda unaojikita katika mashauri ya Kiinjili unaomwilishwa katika neema, uhuru
na utashi kamili.
Licha ya watawa wengi kukata tamaa na kubwaga manyanga katika
maisha haya, lakini bado kuna kundi kubwa la vijana wa kizazi kipya wanataka kujiunga
na mashirika ya kitawa na kazi za kitume, jambo la msingi ni kuimarisha utume wa Kanisa
miongoni mwa vijana. Kuna cheche za ongezeko la miito mitakatifu nchini Ufaransa na
Marekani, huu ni ushuhuda kwamba, kweli Roho Mtakatifu bado anafanya kazi ndani ya
Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na
utume wa Kanisa. Kongamano hili ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani,
changamoto kwa watawa kuishi kikamilifu karama za mashirika yao kwa kuzitolea ushuhuda
wenye mvuto na mashiko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.