Rushwa na ufisadi visipakwe mafuta kwa mgongo wa chupa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawataka Wabunge nchini humo kuhakikisha kwamba,
wanatunga sheria itakayopambana kwa dhati kabisa na rushwa, ufisadi pamoja na wizi
wa mali ya umma, kwani haya ni mambo ambayo kwa sasa ni majanga ya kitaifa na kimataifa.
Kupokea na kutoa rushwa ni kishawishi cha watu wengi ndani ya jamii.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada limechapisha Waraka huu wakati ambapo wanasubiri taarifa
kutoka Serikali ya Canada kuhusu hali na mwelekeo wa vitendo vya rushwa na ufisadi
nchini humo. Hii ni Tume iliyoanzishwa kunako mwaka 2011 ili kuangalia vitendo vya
rushwa na ufisadi vinavyoweze kujipenyeza katika masuala ya ujenzi, vyama vya kisiasa
na makundi ya uhalifu wa kupanga.
Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, taarifa
ya tume hii itatoa pia mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kung'oa vitendo
vya rushwa na ufisadi nchini humo. Rushwa kamwe isipakwe mafuta kwa mgongo wa chupa,
bali ishughulikiwe kikamilifu, kwa kuwawajibisha watu katika ukweli na uwazi. Baba
Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, watu hawana budi kujenga utamaduni wa kuwajibika
ili taratibu rushwa na ufisadi viweze kutokomezwa sehemu mbali mbali za dunia. Juhudi
za kwanza ni ujenzi wa dhamiri nyofu pamoja na kuanza mchakato wa kusafisha matendo
yanayopelekea watu kutaka kujikita katika rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa jamii ijenge utamaduni wa haki, amani
na usawa kati ya watu wake; wananchi wajifunze kuridhika na mapato halali ya kazi
halali wanazofanya. Ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi hatoshi kujikita katika
haki na mshikamano wa kidugu, kwa kugawana kile kilichopo, bali kuwa na sheria makini
zitakazopambana na rushwa, ili hatimaye iweze kuong'olewa katika maisha ya watu.
Kutokana
na kushamiri vitendo vya rushwa na ufisadi, baadhi ya watu wanadhani kwamba, huu ndio
mtindo wa maisha ya kisasa, nje ya mambo haya, wewe umepitwa na wakati! Wananchi wajenge
ujasiri wa kukataa kutoa au kupokea rushwa, iwe ni ndogo au kubwa kiasi gani! Jamii
inawapongeza wale wote ambao hadi wakati huu hawajajihusisha na vitendo vya rushwa
na ufisadi, wao ni mfano bora wa kuigwa na mfungamo wa maisha ya kijamii na kwamba,
inawezekana mtu kuishi bila ya kupokea au kutoa rushwa wala kuwa fisadi.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada limetuma maswali dodoso ili kuangalia hali na mwenendo
wa rushwa na ufisadi nchini Canada, ili kweli hatua makini ziweze kuchukuliwa kama
sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, majanga ya kitaifa na kimataifa kwa
sasa!