Ondoeni vinyago vyenu, ili muonje upendo na huruma ya Mungu!
Toba na wongofu wa ndani katika Kipindi hiki cha Kwaresima vimsaidie mwamini kuwa
mkweli na kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kuomba huruma na upendo wake
katika hija ya maisha ya kiroho. Ni mwaliko wa kumwilisha utajiri wa tunu msingi za
kiroho katika uhalisia wa maisha pasi ya kutafuta visingizio. Kama ilivyokuwa kwa
Nabii Eliya aliyelazimika kujionesha mbele ya Mfalme Ahabu ingawa alihofia usalama
wa maisha yake, hii ndiyo changamoto hata kwa viongozi wa Kanisa kuchunguza undani
wa maisha yao, kusikiliza kwa makini ushauri ambao Mwenyezi Mungu anataka kuwashirikisha
na hatimaye, kuufanyia kazi.
Kimsingi hizi ni kati ya changamoto zinazoendelea
kutolewa na Padre Bruno Secondin kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa
karibu, wakati huu wanapoendelea na mafungo ya maisha ya kiroho huko Ariccia, nje
kidogo ya mji wa Vatican. Wakristo katika ujumla wao wanapaswa kuonesha ujasiri na
uthabiti wa imani hasa pale wanapokabiliwa na changamoto za maisha ya imani. Kanisa
lioneshe ari na ujasiri wa kuwatangazia Watu wa Mungu kweli za maisha pasi na woga
wala makunyanzi wala kutafuta kumfurahisha mtu, kwani ukweli unauma na kuponya!
Viongozi
wa Kanisa wasimame kidete kulinda na kutetea ukweli, hata kama itawabidi kujisadaka
maisha yao, kwani huu ndio utume wa kinabii ambao Mama Kanisa anaalikwa kuutolea ushuhuda
makini, katika hali ya unyenyekevu, daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu
na heshima ya binadamu. Ni wajibu wa Kanisa kuwasaidia, kuwatetea na kuwahudumia maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Kanisa litambua kwamba, rasilimali fedha,
vitu na watu ni kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji na wala si mali ya
mtu binafsi.
Viongozi wa Kanisa wawashirikishe waamini wao katika maisha na
utume wa Kanisa kama alivyofanya nabii Eliya wakati alipokuwa anakabiliwa na majaribu
katika maisha. Pengine umekuwa ni utamaduni kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa kufanya
maamuzi makubwa ya maisha na utume wa Kanisa kwa kuwahusisha watu wachache, lakini,
changamoto za Uinjilishaji mpya zinawataka viongozi wa Kanisa kuthubutu kuishirikisha
yote ya Mungu, pengine kwa njia ya uwakilishi mpana zaidi.
Hapa wazo linaloibuliwa
ni kuanza kujenga utamaduni wa kufanya, kupembua, kupanga na kutekeleza maamuzi kwa
njia ya kuwashirikisha watu. Kanisa litambue mapungufu yake ya kibinadamu na kuwa
na ujasiri wa kuyakiri pasi na woga; liangalie pale ambapo limeshindwa kutenda haki,
ili kuomba huruma na msamaha, tayari kuanza mchakato wa uponyaji wa ndani.
Historia
ya Kanisa anasema Padre Bruno Secondin inaonesha pia kwamba wakati fulani, Kanisa
liliwatesa na kuwanyanyasa watu, pengine madhulumu haya leo hii yanaweza kuwa katika
mtindo tofauti wa maisha kwa maneno au kwa kutumia mitandao ya kijamii. Hapa kunahitajika
toba na wongofu wa ndani, ili kuona ukweli baada ya kuchunguza dhamiri mbele ya Mwenyezi
Mungu, katika uhuru kamili, ili kutoa nafasi kwa Mungu aweze kuwafunda na kuwaponya
kutoka katika undani wa maisha yao.
Padre Secondin anasema, maneno matupu hayawezi
kamwe kujenga na kuimarisha imani, kwani mwelekeo kama huu mara nyingi ndani mwake
kuwa mambo ambayo yamefichika yaani: kiburi, tamaa ya madaraka, mafanikio katika elimu
na huduma; lakini hata katika miungu hii midogo, bado huruma na upendo wa Mungu aliye
hai ni mkuu na unaweza kuunguza na kuwaponya kutoka katika undani wao, kama ilivyokuwa
kwa Nabii Eliya, akafaulu kujenga utambulisho wa Waisraeli kwa njia ya Makabila kumi
na mawili, kwani Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake na yupo daima kwa wale
wote wanaomkimbilia.
Padre Bruno Secondin anawaalika viongozi wa Kanisa kuamsha
tena dhamiri nyofu miongoni mwa Familia ya Mungu, kwa kuwa na mikakati na dira makini
katika shughuli za kichungaji, maisha na utume wa Kanisa; kwa kumwachia Mungu nafasi
katika maisha na mipango yao, daima wakiendelea kumshirikisha kwa njia ya sala.
Nabii
Eliya kama anavyosimuliwa na Mtakatifu Efrehemu ni kielelezo cha Yesu katika Agano
Jipya, hali inayoonesha: Fumbo la Umwilisho, Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na
ufufuko wa Yesu hadi kupaa kwake mbinguni anakoishi mkono wa kuume wa Baba yake wa
Mbinguni. Yesu ni kielelezo na mfano wa maisha yanayojikita katika: ufukara, utii
na useja; mwaliko kwa Familia ya Mungu kuchuchumilia amani na utakatifu wa maisha,
huku wakiendelea kuwa waaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Waamini katika maisha yao,
wajibidishe kuitafuta mbingu, ili waweze kupata maisha ya uzima wa milele.
Padre
Bruno Secondin anasema unga na mafuta aliyotumia Nabii Eliya kufanya muujiza ni kielelezo
cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuwa makini
kwani wanaweza kukumbana na Mbwa mwitu katika maisha na utume wao; wawe wapole na
wanyenyekevu katika kuchunga Kondoo wa Kristo. Wawasaidie waamini wao kuwaosha kwa
maji ya Ubatizo na kuwapaka mafuta ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Kwa ufupi, haya ndiyo mawazo makuu ambayo yanaendelea kutawala katika mafungo yanayotolewa
na Padre Bruno Secondin kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.